Mmiliki wa nyumba ambayo ipo Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mbagala Kuu Magharibi, Temeke Jijini Dar es Salaam, Mawesi Mwiga akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki kuhusu tukio hilo la kutolipwa hela yake ya pango na kufikia hatua ya kuifunga ofisi hiyo mpaka atakapolipwa fedha zake.
Mmoja wa Wajumbe (kulia) akitoa huduma kwa mwananchi huku akiwa amekaa nje baada ya Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mbagala Kuu Magharibi kufungwa kwa madai ya kushindwa kulipa pango. 
Mlango wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mbagala Kuu Magharibi ukiwa umefungwa.


Na Dotto Mwaibale 


OFISI ya Serikali ya Mtaa wa Mbagala Kuu Magharibi iliyopo Kata ya Mbagala Kuu Temeke jijini Dar es Salaam imefungwa na mmiliki wa nyumba kwa madai ya kutolipwa pango la nyumba kwa miezi sita mfufulizo.

Kufungwa kwa ofisi hiyo kumeleta adha kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma katika ofisi hiyo ambapo sasa wahusika wanalazimika kufanya kazi nje chini ya mnazi ilimradi tu watoe huduma kwa wakati kwa wananchi.

Hata hivyo iwapo hatua za makusudi hazitafanyika za kulipa pango hilo hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mvua za masika zitakapoanza kunyesha.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mwishoni mwa wiki mmiliki wa nyumba hiyo Mawesi Mwiga alisema fedha anazodai ni za pango kuanzia Mwezi Julai 2021 hadi Desemba 2021 lakini tangu alipoanza kuwadai amekuwa akipigwa danadana.

Alisema Desemba 22, 2021 aliwaandikia barua ya kuwakumbusha kulipa pango hilo lakini hakukuwa na majibu yoyote zaidi ya kuelezwa aambatanishe mikataba ya upangaji ya miezi ya nyuma hata baada ya kufanya hivyo wameshindwa kumlipa.

"Mpangaji anaposhindwa kulipa pango anakuwa amepoteza sifa za upangaji hivyo baada ya kuona hawanilipi niliamua kuifunga ofisi hiyo hadi hapo watakaponilipa fedha zangu" alisema Mwiga.

Mmoja wa wajumbe wa mtaa huo ambaye alikutwa na mwandishi wetu akitoa huduma akiwa chini ya mnazi alikiri ofisi hiyo kufungwa na mmiliki wa nyumba baada ya kutolipwa hela yake ya pamgo.

"Ni kweli ofisi imefungwa lakini changamoto iliyopo ni mmiliki wa nyumba kutojua ni nani anayepaswa kumlipa ambaye sio sisi bali ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke" alisema Mjumbe huyo ambaye alikuwa akitoa huduma kwa wananchi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya alipopigiwa simu mwishoni mwa wiki ili kuzungumzia suala hilo aliomba apewe muda ili aweze kulifanyia kazi.

Habari zilizotufikia kabla hatujaenda hewani zinadai kuwa sakata hilo limechukua sura mpya baada ya kufuli lililofungwa na mwenye nyumba kuvunjwa na ofisi hiyo kufunguliwa bila ya kufikia muafaka.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: