MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira

 

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira ametimiza mwaka mmoja tokea alivyoapa  tarehe 11 Novemba 2020 kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiwashukuru Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia Mkoa wake wa Kagera hadi Taifa na Wanawake wa Mkoa wa Kagera na Mikoa yote 32 Nchini kwa kumpa nafasi hiyo muhimu.


Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Novemba 11,2021 ambapo alisema katika kipindi chake cha mwaka mmoja tokea amekuwa Mbunge amejikita zaidi katika maeneo nane ya kimkakati ikiwemo Lishe hususani shuleni, Sekta ya Kidigitali kwa maana ya umuhimu wa Serikali kuandaa Digitali Economy Strategy.

Mbunge Neema alisema eneo lingine ni kuhususu Diaspora ambapo Serikali iweke mazingira wezeshi ili watanzania wanaoishi nje ya nchi waweze kuwekeza na kuchangia Maendeleo ya Taifa lao kupitia Special Status yaani Hadhi Maalum 

Jambo jingine ni kupunguza msongamano kwenye magereza kwa kutafuta namna ya kupunguza idadi ya mahabusu.

Alisema pia suala lingine ni uhitaji na umuhimu mkubwa wa upatikanaji wa Taulo za Kike kwa Wanafunzi ambapo kwa mwaka huu 2021 ameweza kutoa msaada wa Taulo za Kike za Kutosha Mwaka Mzima kwa Wanafunzi 5,500 kutoka Mikoa 19 Nchini kwa lengo la kuondosha changamoto ya kukosa shule kila mwezi wakiwa katika Hedhi. 

“Lakini pia umuhimu wa Mahakama ya Familia ili kuweza kuleta haki kwa uharaka zaidi kwenye maeneo ya mirathi na matunzo na kuendeleza mapambano ya kutokomeza malaria na magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipamble” Alisema

Hata hivyo pia alisema katika kipindi hicho suala lingine ni utambuzi wa mchango mkubwa wa Sekta ya Asasi za Kiraia (NGOs) kwenye Maendeleo ya Taifa na hapo wamefanikiwa kufanya Uchaguzi wa Viongozi wa Baraza la Taifa la NGOs (NACONGO) na kuandaa Mkutano wa Mwaka wa NGOs ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa Mgeni Rasmi.

“Kwa nafasi ya kipekee namshukuru Mhe Job Ndugai, kwa namna anayotujengea uwezo na maarifa ili wao Wabunge ili tuendelee kuishauri vizuri Serikali “Alisema Mbunge Neema Lugangira.

Aidha, Mbunge Neema Lugangira alimpongeza Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyongoza nchi na kuleta maendeleo  na yeye kama Mbunge anapata hamasa kubwa ya kuendelea kuishauri Serikali na kuchangia katika Maendeleo ya Taifa letu.

- MWISHO -

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: