Halmashauri zote nchini zimehimizwa kuzingatia mipango bora wa matumizi
ya ardhi ikiwemo kuweka njia za Mifugo zitazowawezesha kwenda kwenye
Malisho, maji na kwenye Masoko Ili kuondokana na migogoro isiyo ya
lazima baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Rai hiyo
ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na
uvuvi Sekta ya Mifugo, Bw. Yusuf Selenge katika mafunzo ya ufugaji
endelevu unaokabili mabadiliko ya tabia nchi yaliyofanyika Mkoani Geita
Novemba 15, 2021.
Akiongea katika mafunzo hayo alisema kuwa
asilimia kubwa ya migogoro inatokana na baadhi ya vijiji kutokuwa na
mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusabisha njia za kupitisha mifugo
ikitumika kwa matumizi mengine.
“hii programu itasaidia sana kwa
sababu imehimiza matumizi bora ya ardhi kwa hiyo Halmashauri wanatakiwa
kutafuta wafadhiri na mapato yao ya ndani kuweza kutekeleza mpango huo
kwa sababu njia za kupitisha mifugo zilikuwepo lakini zimevamiwa kwa
matumizi mengine," alisema
Kuhusu mradi wa utekelezaji wa mradi
wa ufugaji endelevu, Selenge alibainisha kuwa programu hiyo
inatekelezwa katika sekta tatu za kilimo, mifugo na uvuvi ambapo kwa
sasa mafunzo hayo yanatolewa kwa maafisa katika Halmashauri ambao
watawajibika kufikisha elimu kwa wakulima na wafugaji ngazi za vijiji.
Aliongeza
kwa kusema kuwa programu hiyo ilianza kutekelezwa tangu 2015 hadi 2025
ambapo utekelezaji wake unafanyika katika mamlaka ya Serikali za mitaa
kupitia kwa maafisa sita katika halmashauri ambao watawajibika kufikisha
elimu kwa wakulima na wafugaji.
“Halmashauri ndio wanachukua
elimu hii na kuifikisha ngazi ya kata na kijiji, maafisa tunaofanya nao
ni sita kwenye Halmashauri ambao ni Afisa Mazingira, Afisa mifugo na
uvuvi, Afisa kilimo na umwagiliaji, Afisa malisho, Afisa mipango pamoja
na Afisa maendeleo ya jamii,” aliongeza
Aidha Bw. Selenge
aliwahimiza maafisa hao wa Halmashauri kuhakikisha wanawaelimisha
wafugaji njia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo
kuwashauri wananchi kuhimilisha Mifugo yao, kulima Malisho, kuyaboresha,
kuyahifadhi, na kuvuna maji.
Naye, Afisa Mazingira kutoka Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Jeremiah Legela alisema kuwa pamoja na mambo
mengine mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mifugo ikiwemo kutoweka chapa
katika mifugo ambayo imekuwa ikiharibu ngozi na kupunguza ubora.
Aliongeza
kuwa mpango wa sasa ni kutumia njia ya kisasa ikiwemo kuweka hereni
katika masikio na kuiacha ngozi ya mifugo zikiwa na ubora ambapo
unahitajika katika soko hasa viwanda vya ngozi vilivyopo nchini.
Kwa
upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Bi. Mpelwa
James alibainisha kuwa faida waliyoipata katika mafunzo hayo
watahakikisha inawafikia wafugaji ili kuhakikisha wanashiriki kulinda
mazingira hasa katika vyanzo vya maji.
“kitu ambacho nimeondoka
nacho hapa cha kwenda kufanya kwa wafugaji ambao wana mifugo mingi zaidi
ya elfu moja ni kuwahimiza na kuwashirikisha kufanya tathimini za
kimazingira ili kukabiliana na ya athari za mabadiriko ya tabia ya nchi
kwa sababu wasipofanya hivyo kutakuwa na hatari ya kukosa malisho,”
alisema
Aliongeza kuwa hatua hiyo itawaongezea uelewa wananchi
juu ya mabadiriko ya tabia ya nchi na itawajengea uwezo wa kuhimili
mabadiliko hayo ili waweze kuwa na uhakika wa kupata chakula cha mifugo
na kwenye kaya zao kutokana na uzalishaji wenye tija.
Afisa mazingira kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Jeremiah
Legela akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna ya
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi (hawapo pichani) yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita Novemba 15,
2021.Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita
Mkoani Geita Novemba 15, 2021.Kaimu Mkuu wa kitengo cha mazingira Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo)
Bw. Yusuf Selenge (wa nne kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja
na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya geita mara baada ya mafunzo
mafupi ya kuongeza uelewa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
kwa watendaji hao yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya mji wa
Geita Mkoani Geita Novemba 15, 2021.
Post A Comment: