Na Joachim Nyambo
NOVEMBA 17 ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya watoto njiti.Watoto hawa ni wale wazaozaliwa wakiwa hawajakomaa kutokana na ujauzito wao kutofikisha umri wa wiki 37.Siku ya watoto njiti iliyoanza kuadhimishwa tangu mwaka 2011 ilianzishwa kwa nia ya kuelimisha kuhusu kujifungua watoto njiti ambao hawajakomaa na kufikisha wiki 37 tumboni.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani(WHO) na lile la mataifa ya Amerika (PAHO), tatizo la watoto njiti ni chanzo kikubwa cha vifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.WHO pia inasema Takribani watoto milioni 15 wanazaliwa wakiwa njiti kila mwaka.
Katika kuadhimisha siku ya watoto njiti,kaulimbiu zimekuwa zikitolewa kila mwaka zikibeba ujumbe wenye kuleta msukumo kwa jamii kufanya jambo lenye kuongeza ubora wa maisha kwa watoto hawa.
Kwa mfano katika maadhimisho ya mwaka 2016 dunia ilibeba ujumbe kinga ya upofu utokanao na kuzaliwa njiti.Katika kuifanyia kazi kaulimbiu hii siku hiyo ya maadhimisho PAHO ilifanya mkutano kuhusu kuzuia upofu unaosababishwa na hali ya kuzaliwa njiti , ugonjwa ulioonekana kuongoza kwa watoto njiti na ambao unazuilika na kutibika.Mwaka huu kaulimbiu ya siku hii ni Utenganisho sifuri waunganishe mama na mtoto sasa.
Kwa mujibu wa Makala iliyoandaliwa na kurushwa kwenye idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Habari la kimataifa la DW Novemba 15 mwaka 2018,Msongo wa mawazo,lishe duni kabla na wakati wa ujauzito pamoja na mama kubeba mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 zinaweza kuwa sababu za kuzaliwa mtoto njiti.
Vyanzo mbalimbali vya habari vinaeleza kuwa watoto njiti wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vinavyosababishwa na mazingira yanayowazunguka mara baada ya kuzaliwa.Hii inasababisha na kuleta msukumo kwa jamii kuwa makini kwenye malezzi hasa ya awali ya watoto wa kundi hilo.
Ripoti iliyochapishwa 2012 na jopo la wataalamu wawakilishi wa mashirika makubwa ya kimataifa duniani, wasomi, taasisi za kitaaluma na mashirika ya Umoja wa Mataifa, makadirio yanaonyesha uzito wa tatizo la watoto njiti ni kubwa kuliko ilivyoripotiwa mwaka 2010.
Japokuwa vizazi kabla ya muda ni taswira ya tatizo la kidunia, lakini nchi zenye uchumi mdogo hasa zile za Afrika na za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinaelemewa na tatizo hilo.
Ripoti inaonesha miongoni mwa nchi 11 zenye viwango vya juu vya kuzaliwa watoto njiti isipokuwa mbili tu, zipo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2010.
Makala ya Afya iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la Desemba 12 mwaka 2017 yenye kiungo mtandao https://data.mwananchi.co.tz/2017/12/12/vifo-vya-watoto-njiti-pasua-kichwa-afrika-mashariki/ inaonyesha ukubwa wa tatizo la watoto njiti katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.
Makala hayo yanaonesha Nchini Tanzania takwimu zinaonyesha asilimia 13 ya watoto huzaliwa wakiwa na uzito pungufu ambao huchangia kwa asilimia 86 ya vifo vya wachanga.
Ripoti hiyo inasema tatizo linalochangia kusababisha vifo vya watoto hao linalokadiriwa kufikia asilimia 27 ya vifo hivyo, ni pamoja na mtoto kuzaliwa njiti, maradhi ya vimelea vya bakteria, matatizo ya kupumua na kuvuja damu.
Kila mwaka, zaidi ya watoto 210,300 wanazaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito na kati yao, zaidi ya watoto 13,900 hufariki dunia. Kwa takwimu za mwaka 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee, inaonyesha idadi hiyo imeongezeka maradufu kutoka 30 mwaka 2012 hadi kufikia 1,500 mwaka 2016.
Mkuu wa Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wakati huo, Dk Edna Majaliwa anasema licha ya ukubwa wa tatizo, huduma ya Kangaroo imesaidia kwani ukaribu wa ngozi kwa ngozi baina ya mama na mtoto husaidia kupata joto asilia na lisilobadilika kirahisi.
Alisema husaidia pia kupunguza maambukizi ya maradhi kwa watoto, kuongeza hali ya kunyonyeshwa, kupunguza kupaliwa kwa maziwa kunakosababishwa na vifo vya ghafla na upatikanaji wa taarifa ya haraka pindi hali ya mtoto inapobadilika.
Hata hivyo, Dk Majaliwa alisema takwimu zinaonyesha vifo vya watoto njiti vimeendelea kupungua katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2012 hadi 2017 kwa Muhimbili.
“Hii inatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau wa afya ikiwamo kuanzishwa kwa huduma ya Kangaroo katika hospitali za mikoa na rufaa na upatikanaji wa huduma za dharura za kujifungua kwa wajawazito kwenye vituo vya afya (EmONC),” alisema.
Vyanzo vingi vya habari vinaeleza kuwa watoto njiti hukumbwa na ugumu wa kudhibiti kiwangojoto cha mwili.Hupoteza jotomwili kwa urahisi, hivyo wapo katika hatari ya kupata hipothemia katika hali hii.Ndiyo sababu watotot hawa wanaingia kwenye kundi la wanaotakiwa kupewa huduma maalaum.
Huduma hizi ni pamoja na punde baada ya kuzaliwa mtoto kulazwa ngozi yake ikigusana na ya mama, kisha ufuatilishe Utunzaji wa Mama wa aina ya Kangaroo.Blanketi au shuka za ziada zilizotengezwa kwa pamba zinahitajika ili kumfunika mama na mtoto. Jambo muhimu la kukumbuka (linalosahaulika mara nyingi) ni kwamba kichwa cha mtoto kinahitaji kufunikwa vyema.Hii ni kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya jotomwili hutokea kichwani kisipofunikwa vyema.
Wataalamu wanasema chumba anapotunziwa mtoto kinafaa kuwa na kipasha joto cha ziada.Kawisha kumwosha mtoto kwa angalau saa 28 baada ya kuzaliwa, ukitumia maji vuguvugu kila unapomwosha.
Mama wa mtotoanapaswa kuanzisha kumnyonyesha mtoto au kumnywesha kwa kikombe muda mfupi iwezekanavyo baada ya kuzaliwa.Mtoto nayonye kila baada ya masaa mawili.
Utunzaji wa aina ya Kangaroo wa Mama kwa Mtoto(UKM) ni njia ya utunzaji iliyopewa jina kwa kurejelea jinsi wanyama Kangaroo wanavyowatunza ndama wao.Njia hii imetambulika kuwa bora sana katika kuwatunza watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini.Njia hii huhusisha kumshika mtoto huku mwili wake ukigusana na wa mama mchana na usiku. Mtu mwingine hususani baba anaweza kuchukua nafasi ya mama iwapo hawezi kumshika namna hii wakati wote.
Utafiti unaonyesha kuwa njia ya UKM inapotumika, husaidia kudhibiti kima cha mdundo wa moyo na kupumua kwa watoto waliozaliwa kabla ya kuhitimu muhula na waliozaliwa wakiwa na uzani wa chini. Njia hii pia husaidia kupunguza maambukizi na kumwezesha mtoto kuongeza uzani ifaavyo. Njia hii humsaidia mama kwa kuzidisha utoleshaji wa maziwa, na pia kufanikisha kunyonyesha bila kutumia vyakula vya ziada.
Utafiti pia unaonesha njia ya UKM inaweza kuonekana kama njia isiyo ya kawaida ya kumtunza mtoto. Kwa hivyo, ni muhimu kuchukua muda unapomshauri mama, baba na familia kuhusu vipengele vya njia hii na manufaa yake. Mama na familia wanapaswa kushawishika na kukubali kutumia njia hii kwa siku nyingi mfululizo.Baba na watu wengine wa familia pia wanapaswa kuwa tayari kutoa usaidizi wa kimwili na kihisia kwa mama anapotumia njia hii.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa manufaa ya UKM ni pamoja na kuendeleza kunyonyesha, kudhibiti jotomwili la mtoto, kuongeza uzani mapema, kupumua vyema zaidi na upungufu wa kima cha maambukizi.
Watoto wanaotumia huduma hii ya UKM wanapumua kwa ubora zaidi na uwezekano kukoma kupumua ni wa kima cha chini. Njia hii pia humkinga mtoto dhidi ya maambukizi.
Inashauriwa kuhakikishe kuwa mama hana matatizo au maradhi yoyote yanayoashiria kuwa anakosa nguvu za kutumia njia hii bila kusaidiwa.Ikiwa anakumbwa na matatizo haya, inapaswa kubaini kama baba au jamaa yeyote wa familia anaweza kushirikiana na mama kutoa utunzaji huu au kumtunza mtoto kwa njia hii wakati wote iwapo mama anaugua.
Njia hii inashauriwa pia kuendelea kutumiwa kwa kipindi kirefu kama inavyowezekana au mpaka mtoto ahitimu muhula wa kuzaliwa (wiki 40) ama mpaka mtoto apate uzani wa gramu 2,500. Iwapo mtoto ana uzani unaozidi gramu 1,800 na kiwango chake cha jotomwili ni dhabiti, hana matatizo yoyote ya kupumua na ananyonya vizuri, anaweza kulishwa kupitia UKM kabla ya wiki 40.
Hatimaye, ukifuata maagizo haya na kuwasaidia familia zako kutunza watoto wao waliozaliwa kabla ya wakati wao ni hakika kuwa utaokoa maisha ya watoto wengi wachanga. Kunalo jambo muhimu kuliko hili.
NOTE-Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao.
Post A Comment: