Julieth Ngarabali,   Kibaha.  


Jeshi la Polisi Mkoani Pwani limebaini kuwepo makampuni ya Ulinzi binafsi yanayotumia silaha zisizoruhusiwa kutumika katika ulinzi. 


Kamanda wa Polisi Pwani Wankyo Nyigesa amesema wamebaini kampuni hizo nyingi bado zinatumia silaha aina ya gobore, rifle na short gun ambazo ni kati ya silaha zisizoruhusiwa kutumika katika ulinzi.


Wankyo ametoa rai wamiliki wa kampuni hizo wazihuishe na kusajili silaha zinazopendekezwa ama zinazohitajika ambazo ni short gun pump action .


Amesema hayo  mjini Kibaha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa zoezi la kusalimisha silaha kwa hiari ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa mambo ya ndani George Simbachawene aliyeelekeza Oktoba 30 mwaka huu kuwa  kika mwananchi anaemiliki silaha kinyume cha sheria aisalimishe kwa hiari katika vituo vya polisi vilivyopo karibu, serikali za mitaa, vijiji na kata.


Kamanda huyo wa Polisi Pwani amebainisha kuwa kampuni  itakayoshindwa kuhuisha silaha zake itafutiwa usajili wa kua kampuni ya ulinzi.


Ameongeza kuwa zoezi la kusalimisha silaha kwa hiari limeanza Novemba mosi na litaisha tarehe 30 mwezi huu na baada ya tarehe hiyo msako utafanyika na atakayebainika anamiliki silaha kinyume na sheria hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake .


"Jeshi la Polisi Pwani linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa ulinzi na usalama wao umeimarishwa na waendelee kufanya kazi zao kwa amani na utulivu "amesema Wankyo.

Share To:

Post A Comment: