Afisa Udhibiti Ubora (TBS), Bw. Stanford Matee akitoa elimu ya namna ya kutambua bidhaa zilizothibitishwa ubora na umuhimu wa kuhakikisha muda wa matumizi wa bidhaa kwa wananchi wakati wa kampeni ya elimu kwa umma eneo la stendi wilayani Lushoto.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko (TBS), Bi. Gladness Kaseka akitoa elimu ya viwango kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Lushoto wakati wa kampeni ya elimu kwa umma wilayani Lushoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Bi. Ikupa Mwaisyoge (wa kwanza kushoto) akiwakaribisha maafisa wa TBS kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma katika wilaya ya Lushoto pamoja na kupokea zawadi ya kava za tairi kwa ajili ya kutangaza shughuli za TBS walipoenda kumtembelea ofisini kwake.
*******************************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu ya viwango vya ubora wa bidhaa katika wilaya ya Lushoto ambapo imeweza kukutana na wafanyabiashara mbalimbali pamoja na wanafunzi na kuwahimiza kutumia bidhaa zenye ubora ili kuweza kumlinda mlaji.
Akizungumza mara baada ya kutembelewa na maafisa wa TBS ofisini kwake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Bi.Ikupa Mwaisyoge ameipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wananchi katika ngazi ya Wilaya.
“Elimu hii mnayoitoa TBS itaongeza ufahamu na kuhakikisha suala la uuzaji wa bidhaa hafifu sokoni linapungua kama sio kuisha kabisa” Alisema Bi.Ikupa.
Pia aliwaomba TBS kutoa mafunzo katika vikundi vya wajasiriamali wilayani Lushoto ili waweze kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutumia alama ya ubora. Alisema Bi. Ikupa
Pamoja na hayo TBS imetoa elimu ya viwango pia kwa wanafunzi na walimu wa shule za Sekondari ya Lushoto na Shambalai ; shule za msingi ya Yoghoi na Mbula pamoja na maeneo ya wazi na stendi wilayani humo ambapo muitikio wa uelewa wa elimu hiyo ulikuwa mkubwa. Elimu hii itaendelea kutolewa katika wilaya za Rombo na Hanang katika siku za karibuni.
Post A Comment: