Mtaalam wa Kilimo wa Taasisi  isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania, Ezekiel Shirima (kushoto) akimkabidhi mti Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Ramadhani Ighondo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga maadhimisho ya wiki moja ya kuanza msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2021/ 2022 yaliyofanyika Kijiji cha Msange Wilaya ya Singida mkoani hapa alipotembelea banda la taasisi hiyo  kwenye maadhimisho  hayo.   .

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Eliya Digha akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo alipotembelea banda la taasisi hiyo kwenye hafla hiyo.
Wananchi wakiwa kwenye banda la taasisi hiyo wakipata maelezo.
Wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakiwa kwenye banda lao wakati wa hafla hiyo.
Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Singida Ibrahim Mghama, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
 Msimamizi wa miradi wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Veliksi Haji akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
    Afisa Mtendaji wa kata hiyo Grace Samson akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

     Mkazi wa Kijiji cha Msange Neema Matiti akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Wananchi wakiwa wamebeba miti waliopewa na taasisi hiyo kwenye maadhimisho hayo.

Picha ya pamoja.


Na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Trees for the Future Tanzania inayojishughulisha na kilimo mseto, kilimo endelevu kwa wakulima wenye kipato cha chini vijiji ili kutokomeza njaa, Umaskini na Ukataji wa miti yenye makao yake makuu mkoani Singida imepanda miti zaidi ya 8 milioni kwa ajili ya kutunza mazingira.

Hayo yalisemwa na msimamizi wa miradi wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Veliksi Haji katika hafla ya kufunga maadhimisho ya wiki moja ya kuanza msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2021/ 2022 yaliyofanyika Kijiji cha Msange Wilaya ya Singida mkoani hapa jana.

Haji alisema tangu shirika hilo lianze kufanya kazi mkoani hapa mwaka 2016,  mwaka 2019 lilifanikiwa kupanda miti 2.5 milioni, mwaka 2020 miti milioni 3.2 na mwaka huu wanatarajia kupanda miti milioni 2.8.

" Hivyo tangu shirika hili lianze kufanya kazi limepanda miti zaidi ya 8 milioni ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu ndani ya Mkoa wa Singida," alisema Haji.

Alisema katika miti hiyo iliyopandwa ipo miti ya matunda, mbao, uzio, miti ya kurutubisha ardhi na malisho kwa ajili ya mifugo. 

Mratibu wa Shirika hilo mkoani hapa  Ibrahim Mghama alisema shirika hilo mpaka sasa lina miradi saba na linafanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika kata 13, Mkalama kata 2, Iramba kata 2 na Ikungi kata 2.

Alisema shirika hilo limewafikia wakulima wa moja kwa moja 3,192  na wale wasio kuwa wa moja kwa moja wakiwa ni 15,960.

Mghama alisema lengo la shirika hilo ni kupunguza umaskini wa kipato kwa kufanya shughuli endelevu za upandaji wa miti ili kukomesha njaa, umaskini wa kipato na kuboresha afya za wanajamii.

Alisema shirika hilo katika kutekeleza kazi zake linafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Wizara ya Kilimo, Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Tumbi Tabora, Clinton Foundation, Helvetas, Jeshi la Magereza Tanzania na mashirika mengine mengi yasiokuwa ya Kiserikali.

 Alisema shirika hilo sasa limepanuka  na kuwa lipo mikoa ya Tabora na Iringa na kuwa katika Mkoa wa Singida kuna miradi saba, miradi minne mkoani Tabora na mmoja mkoani Iringa.

Mkazi wa Kijiji cha Msange Neema Matiti alilipongeza shirika hilo kwa kuwapatia mafunzo hayo hasa ya upandaji wa miti ya aina mbalimbali na kuwa sasa wamejua umuhimu wa jambo hilo.

Alisema nafunzo hayo hayajawanufaisha wao peke yao bali na wenzao wa Kata ya Maghojoa.

Afisa Mtendaji wa kata hiyo Grace Samson alisema mafunzo waliopata wananchi wa kata hiyo yatawasaidia kutunza mazingira kwani hapo awali walikuwa wakikata miti hovyo kwa kuwa walikuwa hawana elimu yoyote ya utunzaji wa mazingira.

Alisema kutokana na elimu hiyo anaamini itazaa matunda na kata hiyo itakuwa ya kijani na watu wengine watakwenda kujifunza dhana nzima ya kutunza mazingira.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: