Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema mpaka kufikia 2025 barabara za Halmashauri ya Wilaya Moshi zenye urefu wa km 23.4 zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa daraja la Rau lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mapema leo tarehe 15.10.2021
Amezitaja barabara hizo kuwa ni kutoka Rau-Mamboleo kwenda Materuni yenye urefu wa km 10 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami pamoja na barabara ya kutoka Mamboleo- Rehani kwenda Shimbwe yenye urefu wa km 13.4.
Pia amesema kuwa barabara ya kutoka Rehani kwenda Mruwia yenye urefu wa km 4 itachongwa na kuwekwa moram.
Daraja la Rau lililowekewa jiwe na msingi leo linajengwa kupitia Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA) na liko mpakani mwa kata za Rau na Uru na linaunganisha kata za Uru Kaskazini, Kusini, Shibwe na Uru Mashariki.
Ujenzi wa daraja hili unarejesha mawasiliano yaliyokatika kwa takribani mwaka mzima kwa Wananchi wa Kata ya Rau na Uru baada ya daraja lililokuwepo awali kusombwa na maji yaliyosabishwa na mvua za vuli zilizonyesha April,2020.
Daraja hili linajengwa kwa gharama ya Shilingi Mil. 910 litakamilika Januari,2022 na litakua na uwezo wa kupitisha mizigo yenye tani 50.
Post A Comment: