Na. Tito Mselem, DSM


Imeelezwa kuwa, uwepo wa Rasilimali madini nchini Tanzania yametokana na jiolojia iliyopo nchini humu ambayo ni Baraka za Mwenyezi Mungu aliyoipatia Nchi hiyo sababu madini ni asili na wala hayatengenezwi.


Hayo, yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya alipowasilisha Mada kwenye Kongamano la Wiki ya Nishati na Madini lililoandaliwa na Mwananchi Communication Limited katika ukumbi wa Marque uliopo ndani ya hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.


Prof. Manya amesema Tanzania ni nchi ya tano barani Afrika kwa uzalishaji wa Madini ya dhahabu ambapo utafiti wa Madini Nchini Tanzania ulianza tokea mwaka 1890 chini ya ukoloni wa Wajerumani katika milima ya Saragura Mkoani Geita lakini Mgodi wa kwanza wa madini ya dhahabu ni Sakenke Mine ulionza kazi mwaka 1909.


“Tumegundua kuwepo kwa ukuaji mkubwa wa Sekta ya Madini ambapo mwaka 2019 Sekta ya Madini ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa ukuaji kwa asilimia 17 pia, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa ulitoka asilimia 4.8 Mwaka 2017 kwenda asilimia 6.7 mwaka 2020, hivyo ifikapo mwaka 2025 tunataka tuwe tumefikia asilimia 10 ya mchango wa sekta katika Pato la Taifa,” amesema Prof. Manya.


Aidha, Prof. Manya amesema, uwepo wa idadi kubwa ya watoa huduma wa Kitanzania katika shughuli za Madini kumechochewa kwa kiasi kikubwa na usimamizi wa Sheria ya Madini na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania.


Prof. manya amesema,  katika kipindi cha Mwaka 2020/2021 jumla ya kampuni za watoa huduma katika shughuli za madini 961 sawa na asilimia 66 zilikuwa ni za Kitanzania na idadi ya kampuni za kigeni zilikuwa 506 sawa na asilimia 34.


“Wizara imekuwa ikisisitiza wamiliki wa leseni za madini kutoa kipaumbele kwa bidhaa  au  huduma  zinazotolewa na watanzania na kuhakikisha kuwa bidhaa au huduma pekee zinazotolewa na kampuni za kigeni ni zile ambazo hazipatikani Nchini”, amesema Prof. Manya.


Pia, Prof. Manya, amesema, Benki mbalimbali zilizopo Nchini zimekuwa zikishiriki katika kuwezesha shughuli mbalimbali katika  Sekta  ya  Madini ambapo benki hizo zimekuwa zikitoa  mikopo  kwa kampuni mbalimbali zinazofanya shughuli za uchimbaji na biashara ya Madini.


Kufuatia hatua hiyo, Benki ya NMB imeanzisha Madini club ambapo wachimbaji wa madini wanakopeshwa vifaa vya uchimbaji badala ya pesa taslimu na pia, kumekuwepo na  muunganiko wa Benki kupitia chama cha Mabenki (Tanzania Bankers Association) na kuweka nguvu pamoja endapo mkopo unaotakiwa ni mkubwa kiasi kwamba Benki moja haina uwezo wa kutoa mkopo huo.


Baadhi ya Benki zinazoshiriki katika utoaji wa mikopo kwenye shughuli za migodi ni pamoja na NMB Benki, CRDB Benki, NBC Benki, Stanbic Benki. Ecobank na Standard Chartered Benki.


Prof. Manya amesema hadi kufikia Mwezi Septemba 2021, jumla ya Masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 59 vilikuwa vimeanzishwa nchini ambapo Tume ya Madini inaendelea kusimamia biashara ya Madini katika masoko hayo ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa ufanisi.


Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, 2021 jumla ya mapato yaliyotokana na mauzo ya Madini katika masoko ni Shilingi bilioni 40.74. Katika fedha hizo, kiasi cha Shilingi Bilioni 34.87 zilitokana na mrabaha na Shilingi Bilioni 5.87 zilitokana na ada ya ukaguzi.amesema Prof. Manya.


Lengo la Kongamano hilo ni kujadili masuala ya Kisera, Sheria, Mikakati ya Masoko, Fursa za Uwekezaji kutoka nje ya Nchi, suala la Ushiriki wa Watanzania kama Wadau wa Maendeleo na kuangalia Mustakakali wa Nchi baada ya Miaka 60 ijayo.

Share To:

Post A Comment: