Na Dotto Mwaibale, Ikungi
SERIKALI wilayani Ikungi mkoani Singida imesema Maadhimisho ya Siku ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere yatakayofanyika mwakani yatakuwa ya kipekee ambapo midahalo ya kuwafundisha wanafunzi kuhusu maendeleo ya Taifa itatolewa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Bonanza la michezo mbalimbali ikiwa ni Maadhimisho ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere ambayo yalifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ikungi.
" Ndugu zangu niwashukuru ninyi nyote mliojitokeza kuja kushiriki michezo mbalimbali tangu asubuhi kwa ajili ya kumbukizi hii ya kuadhimisha siku ambayo mhasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki," alisema Muro.
Muro aliwashukuru washiriki wote wa bonanza hilo wakiwemo viongozi wa wilaya hiyo, wanafunzi pamoja na Afisa Michezo wa wilaya hiyo Rachel Maliwa kwa kuratibu bonanza hilo.
Alisema wanapo maliza kumbukizi hiyo wao kama Serikali ndio mwanzo wa maandalizi mapya ya kuandaa Tamasha lingine la mwaka ujao kwani alifika kwenye bonanza hilo kuona na kujifunza.
Alisema maandalizi ya kumbukizi nyingine ya Mwalimu Nyerere inayokuja wataanza maandalizi yake mapema na kwa muda mrefu wakisaidiana na Walimu, Afisa Utumishi, Afisa Michezo, Afisa Elimu Sekondari na Msingi.
Alisema katika tamasha hilo itafanyika midahalo ya kitaaluma baada ya kutengeneza mada mbalimbali watakazopewa wanafunzi ambazo zitaelezea mtazamo na maendeleo ya Taifa na kuzishindanisha shule zote za Sekondari zilizopo kwenye wilaya hiyo na washindi watapatiwa zawadi zitakazopendekezwa.
Alisema michezo itaanza wiki mbili kabla ya siku ya maadhimisho hayo kwa kuzishindanisha timu za shule na za mitaani na siku ya kilele watatoa vikombe, zawadi na kwa wanafunzi watapatiwa vyeti na kwa shule itakayofanya vizuri sana itapatiwa zawadi nono na ya kipekee ambayo ni siri yake na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Muro alitumia nafasi hiyo kuwataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha mambo mengine yote yatakayoweza kuwakwamisha wasiweze kumaliza masomo yao na kushindwa kutimiza ndoto za maisha yao.
Afisa michezo wa wilaya hiyo Rachel Maliwa alisema katika kumbukizi ya Mwalimu Nyerere waliona wafanye bonanza la michezo mbalimbali kukimbia (Jogging) kilometa mbili, mazoezi ya viungo, mpira wa miguu, kikapu, Netball na mingine mingi ambayo ilichezwa na Watumishi wa Serikali Kuu, Halmashauri na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ikungi.
Alisema bonanza hilo lilifanyika sambamba na upimaji wa afya kama kupima uzito, urefu, damu, Ukimwi, uchangiaji wa damu salama na chanjo ya Uviko 19.
Alisema kazi hiyo ya upimaji wa afya ilifanywa na Wafanyakazi kutoka Idara ya Afya wilaya humo.
Wanafunzi wa Sekondari ya Ikungi Glory Malecela na Rehema Peter wakizungumza kwa nyakati tofauti katika bonanza hilo walisema michezo inawafanya wafurahi, kujumuika na watu mbalimbali, inawafanya kuwa vizuri katika masomo na wakatoa shukurani zao kwa waandaaji wa bonanza hilo.
Post A Comment: