Na Joachim Nyambo,Mbeya. 


NAIBU Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto,Mwanaidi Ali Khamis amekipongeza Chuo cha Maendeleo ya jamii Uyole kilichopo jijini Mbeya kwa kuanzisha Programu ya wanagenzi inayowapa fursa wanafunzi wa chuo hicho kujifunza ujuzi mwingine nje ya masomo yao na kuwaandaa kuwa wajasiriamali. 


Naibu waziri huyo alitoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua bidhaa mbalimbali za wanagenzi waliopata mafunzo ya ujasiriamali wa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali wakiwa chuoni hapo na sasa baadhi yao wamehitimu na kabla ya kupata ajira kutokana na taarima waliyosomea wamekwishaanza uzalishaji wa bidhaa na kuaanza kujipatia kipato. 


Mwanaidi alisema uwepo wa program hiyo una faida kubwa si kwa wanachuo pekee bali pia jamii inayowazungunga na hata watakayokwenda kuitumikia watakapoajiriwa kwakuwa watatumia ujuzi wa uanagenzi kuwafundisha wananchi njia mbadala za kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali. 


“Nimepata maelezo na kuona aina ya mafunzo yaliyotolewa siyo tu kwaq nadharia bali kwa vitendo  vinavyowajengea uwezo wanachuo kujiajiri na kuajiriwa.Hawa tayari wanaweza kujiajiri wenyewe na wengine watakuja kuajiriwa serikali itakapotoa nafasi.” 


Alipongeza pia jitihada zinazofanywa na chuo hicho katika kupanua wigo ndani ya jamii wa kutambua fursa na changamoto  na kuendelea kutafuta mbinu za kiubunifu kwa kufanya tafiti na kuleta mawazo bunifu  kupitia Kituo cha Ubunifu cha chuo. 


Miongozi mwa mambo aliyopongeza katika hilo ni kuwepo kwa taarifa zinazopatikana kwenye kituo hicho alizosema zinaweza kusaidia wataalamu kuja na njia mbalimbali za kuwasaidia wakulima na wafugaji kwenye kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili. 


Aliusihi uongozi wa chuo sambamba na kuwatafutia soko la uhakika wabunifu na wajasiriamali pia watumie fursa ya uwepo wa Kituo cha Ubunifu kwa kuzifikisha taarifa zinazozalishwa kituoni hapo kwa jamii ili iweze kuzitumia na kuzidi kukitangaza chuo. 


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho,Rajab Sadick Kaleranda alisema uanagenzi ni program nyingine ambayo chuo kinatekeleza kwa lengo la kuwawezesha wahitimu na wanachuo waliopo katika vyuo vya maendeleo ya jamii kuweza kupata ujuzi na uzoefu wa kazi katika Taasisi na mashirika ya kiserikali na binafsi. 


Kaleranda aliyataja mashirika wanayoshirikiana nayo kwa sasa katika program hiyo kuwa ni pamoja na Shirika la simu la TTCL,Chuo cha ufundi(VETA),Caritas,ADP PAMOJA NA Bonde la maji la Ziwa Victoria(LVBWB) ambapo taasisi hizo zimeweza kupokea wanagenzi kutoka mpango huo na muda wa uanagenzi ni miezi mitatu. 


“Tumeanzisha mpango huu kwa lengo la kuwasaidia wahitimu na wanafunzi waliopo chuoni kupata ujuzi na uzoefu wa kazi ili pindi fursa za ajira na kujiajiri zinapotokea waweze kuwa na sifa za kuajirika na kujiajiri kwakuwa watakuwa na uzoefu.” Alifafanua Kaleranda. 

Share To:

Post A Comment: