Na Joachim Nyambo,Rungwe.
UKOSEFU wa nyumba kwaajili ya kuishi watoto wanaozidi umri wa miaka miwili umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazokikabili kituo cha kulelea watoto yatima cha Igogwe kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa Katibu wa Hospitali binafsi ya Igogwe na Msimamizi wa kituo hicho,Nehemia Mbugi miundombinu iliyopo kituoni hapo ni kwaajili ya watoto wachanga pekee hivyo inawapa ugumu kuwalea watoto wanaofikia umri wa kuanzia miaka miwili.
Akitoa taarifa ya kituo hicho,Mbugi alisema watoto wanaozidi umri wa miaka miwili wanahitaji malezi,matunzo,malazi,chakula na mambo mengine ambayo ni tofauti na watoto wachanga lakini wanalazimika kuendelea kuwa na watoto hao kwakuwa hawana ndugu na kituo hakina mahali pa kuwapeleka.
Alisema kutokana na ukosefu wa nyumba,mpaka sasa watoto waliozidi umri wa miaka miwili wamekuwa wakilala katika nyumba za watawa na wengine wanawapeleka kwa muda kwenye kituo cha Mahango kilichopo wilayani Mbarali mkoani hapa huku akisema kituo kilikwishatengeneza ramani ya nyumba mpya kwaajili ya watoto wakubwa lakini upatikanaji wa fedha kwaajili ya ujenzi umekuwa tatizo.
Mbugi aliitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa fedha za kuendeshea kituo ikiwemo kulipa mishahara ya wahudumu akisema kwa sasa kituo hicho chenye jumla ya watoto 34 kina jumla ya wahudumu 16 wa kuajiriwa na watatu wanaojitolea ambapo zinahitajika fedha kiasi kisichopungua Shilingi milioni sita kwa mwezi kulipa mishahara.
Alisema pia mahitaji mengine ya kituo kama kununua umeme,sabuni za usafi,maji na nyinginezo zinahitaji pesa ambazo kiujumla hawana chanzo chochote cha kuzipata zaidi ya kutegemea malipo ya wagonjwa kutoka hospitalini.
Uchakavu wa mashine za kufulia nguo za watoto ni changamoto nyingine iliyopo inayohitaji ufumbuzi kwakuwa kituo kimekuwa kikitumia mashine zilizochakaa zilizonunuliwa na wazungu miaka ya 1970 wakati kinaanzishwa.
Akizungumzia changamoto hizo alipotembelea kituo hicho,Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto,Mwanaidi Ali Hamisi aliagiza Ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri hiyo kukaa na kukitafutia kituo eneo la kujenga jengo jipya.
Sambamba na kuwasilisha zawadi mbalimbali kwa watoto kituoni hapo,pamoja na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizopo Mwanaidi aliwapongeza watumishi kwa kuendeleza malezi kwa watoto kwa upendo huku akikemea vikali wanaofanya vitendo vya kutupa na kuelekeza watoto na kutaka sheria kuchukua mkondo wake kwa wanaobainika.
“Hii si kazi ndogo mnayoifanya hapa.Ninyi ndiyo mama na ndiyo baba wa watotot hawa.Mmeendelea kuwa na upendo na kuwalea.Ni kazi kubwa ambayo mshahara wake si rahisi kuupata hapa duniani bali Mbinguni.Endeleeni na moyo huu wakati tukiangalia namna ya kutatua changamoto zenu.” Aliwatia moyo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Rungwe,Dk Vicent Unai pamoja na kuahidi kukaa na mkurugenzi ili kuangalia uwezekano wa kupata eneo kwaajili kukipa kituo hicho aliahidi pia kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wabunge ili kuwashirikisha changamoto zilizopo na kuzitatua ikiwemo ununuzi wa mashine ya kufulia nguo za watoto.
PICHA-Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Mwanaidi Ali Khamis akikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto wanaoishi kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Igogwe kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya alipokuwa ziarani mkoani humo.(Picha na Joachim Nyambo)
Post A Comment: