MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe (UWT) Scolastika Kevela ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart amewataka wakurugenzi wapya walioteuliwa kwenda kuchapa kazi kwa juhudi ili kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza Dar es Salaam,Mama Kevela alisema ni vyema wateuliwa hao wapya wakatambua kuwa wameaminika hadi kupewa nafasi hizo  hivyo hakuna sababu yoyote ya wao kwenda kuleta uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuangusha Rais Samia aliyewateua.

“Rais ametimiza wajibu wake  kikatiba wa kuwateua hivyo ni vyema waende wakachape kazi kwa weledi ili kumsaidia katika  majukumu mbalimbali ya ujenzi wa Taifa na kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika maeneo waliyopangiwa” amesema Mama Kevela

Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa wiki alifanya uteuzi wa wakurugenzi 184 wakiwemo wapya 69 ambapo kati yake wanawake ni 33 sawa na asilimia 48  huku katika idadi ya jumla ya wakurugenzi wote 184 wanawake wakiwa 55 sawa na asilimia 29.

Akilizungumzia hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Ummy Mwalimu mbali na kumshukuru Rais Samia kwa kuteua wanawake nusu ya idadi ya wakurugenzi wapya, alisema hatua hiyo ni kubwa kwa wanawake na kwamba Rais anastahili pongezi.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kupigania usawa katika nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini, idadi hii ya wakurugenzi wapya aliowatua inazidi kutupa motisha na chachu ya kuongeza bidii katika kazi sisi kama wanawake, kikubwa tuendelee kuchapa kazi ili kumsaidia katika utendaji wake” alisema Ummy

Aidha akilizungumzia hilo Mama Kevela alisema yeye kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe uteuzi wa idadi ya wanawake 33 katika nafasi hiyo ya ukurugenzi imemfurahisha  kwa kuwa inazidi kuondoa pengo la uwiano kati ya wanawake na wanaume huku akiwataka wanawake hao kwenda kuchapa kazi ili kumtia moyo Rais Samia.

Alisema Rais Samia amewaamini kwa kiasi kikubwa hadi kuwachagua katika nafasi hizo na kuwaacha wengine wengi waliopo na kwamba kwa sasa jukumu lao kubwa ni kwenda kumuwakilisha katika nafasi walizopewa ili kuudhihirishia umma kuwa walistahili katika nafasi hizo.


ends

Share To:

Post A Comment: