Na Karama Kenyunko

UPANDE wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iuelekeze upande wa Jamuhuri kuhakikisha wanaleta maelezo ya mashahidi ili washtakiwa waweze kujua hatma yao

Hatua hiyo imefikwa baada ya mshtakiwa Mbowe na wenzake kuunganishwa kwa kusomewa mashtaka yao  pamoja na wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla ambapo baada ya kumaliza kusoma akadai kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba aliwataka upande wa Jamuhuri kurejea mwenendo wa kesi wa Julai 26 ambayo Mbowe alisomewa mashtaka peke yake ambapo walidai upelelezi umekamilika.

Kufuatia hali hiyo Wakili Hilla akadai upelelezi umekamilika ila walisema haujakamilika kwa sababu jalada la kesi hiyo liko kwa DPP kwa ajili ya kuandaliwa maelezo ya mashaidi.

Akijibu hoja hiyo wakili Kibatala ndipo akaiomba mahakama wauelekeze upande wa Jamuhuri kuhakikisha mwenendo wa kesi hiyo unanyooka itakapopangiwa tarehe nyingine wajipange kuleta maelezo ya mashahidi ili washtakiwa wajue hatma yao.

Amedai, upande wa mshtaka wanaiudisha kesi nyuma na kisheria siyo sawa. "Tunawasikia wapelelezi wakiuarifu umma kuwa upelelezi umekamilika na wanaenda mbali na kusema washtakiwa wametenda mambo ya  ovyo ovyo hivyo haya wanayoyasema leo ni kutuchanganya, na muhimu zaidi ni kuichafua mwenendo wa kesi" amesema Kibatala.

Hakimu Simba akasema ni vema mambo yafanyike haraka, hoja ya Kibatala inaweza kuwa na mashiko tujiweke vizuri.

Akijibu tena hoja hizo Hilla amedai, kwa ujumla upelelezi umeishafungwa kilichobaki ni DPP kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unawakilishwa na mawakili wa serikali waandamizi Pius Hilla, Christopher Msigwa na Sylivia Mitanto huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na jopo la mawakili tisa wakiongozwa na  wakili wa utetezi Peter Kibatala, Jonathan Mndeme, John Malya na Frederick Kihwelo. 

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine ni  Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

Washtakiwa wote wanakabiliwa na shtaka la kula njama ya kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya Umma. Huku Mbowe peke yake akikabiliwa na shtaka la kufadhili vitendo vya kigaidi, na washtakiwa Hassan, Kasekwa Lingwenya wakidaiwa kupokea pesa kutoka kwa Mbowe kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi.

Pia mshtakiwa Kasweka anadaiwa kukutwa na silaha aina pisto na risasi tatu huku mshtakiwa Hassan akikutwa akitumia sare na vifaa vya jeshi.










Share To:

Post A Comment: