Jane Edward,Arusha


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, amesimamisha shughuli za uchimbaji wa moramu katika kijiji cha lengijave Kutokana na uharibifu wa miundombinu ya tanesco wakati wa shughuli hizo za uchimbaji hali inayofanya nguzo za umeme kuanguka.


Akizungumza katika ziara ya kushtukiza mara baada ya kukagua eneo hilo Mongela amesema kuwa shughuli za uchimbaji haziwezi kuendelea kutokana na uharibifu wa nguzo za umeme ambazo zinatokana na mradi wa umeme wa nchi mbili Kati ya Kenya na Tanzania


"Mimi najua kuwa shughuli hizi za uchimbaji kuna watu wanajipatia kipato lakini hatuwezi kuhujumu serikali na kuhujumu shughuli za nchi yetu kutokana na uchimbaji huu holela,sasa wataalamu wakae chini waangalie upya ili tusiharibu mradi huu mkubwa"Alisema Mongela


Msimamizi wa mradi mradi wa njia ya usafirishaji umeme msongo wa kilovolt 400 Tanzania na Kenya, Mhandisi Laurence Juae amempongeza Mkuu wa Mkoa huyo kwa kufanya maamuzi hayo ya kufunga shughuli za uchimbaji kwani hali hiyo ilikuwa ikisababisha madhara makubwa na kuchelewesha nguzo kujengwa kwa wakati .


"Unakuta nguzo imejengwa vizuri lakini wachimbaji wakija wanachimba chini hali inayofanya nguzo kutitia na hatuwezi kwenda mbele inabidi turudi kurekebisha kwanza,kwahyo inakuwa changamoto kweli" Alisema Juae


Ameongeza kuwa mradi huo una kilomita 414 kutoka Singida mpaka Namanga ambapo kwa ujumla mradi utajengwa kilomita510 ambapo ukikamilika utasafirisha megawatt 2000 kwa wakati Mmoja


Akifafanua kuhusu faida za mradi huo amesema kuwa mradi huo ukikamilika utakuza uchumi katika vijiji ambavyo mradi huo utapita,ajira kwa vijana itapatikana huku akiwataka wananchi kutunza mradi huo na kuacha kuhujumu miundombinu hiyo ili kuwezesha mradi kukamilika kwa wakati.


Naye Afisa usalama Tanesco Arusha John Chirare amesema kuwa kamwe shirika halitamvumilia mtu akionekana kuharibu mradi huo ambao umegharamiwa kwa fedha nyingi.


Amefafanua kuwa kumeibuka tabia ya wananchi kujishughulisha na wizi hasa maeneo ambayo mradi huo unapita na kuwataka wananchi kuwa mabalozi wa kuwafichua wezi hao wanaohuhumu shirika hilo.


Mwisho.....

Share To:

Post A Comment: