Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA
YA Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kumuunganisha Mwenyekiti wa CHADEMA
Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa kwa tuhuma za kesi ya
uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi kutokana na mawasiliano mabaya
kwenye Ukumbi wa mahakama ya mtandao ( Video Conference) kati ya Kisutu
na Gerezani Ukonga walipo Washtakiwa.
Mapema leo Agosti 5, mwaka
2021, kesi hiyo ambayo imepangwa kusikilizwa kwa ajili ya mtandao
ilikuja kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba
na kumuunganisha Mbowe na wenzake baada ya yeye kusomewa mashtaka peke
yake, lakini ilishindikana baada ya Mbowe na wenzake kushindwa kupata
mawasiliano mazuri kutoka mahakamani.
Katika kesi hiyo, upande wa
mashtaka unawakilishwa na Wakili wa Serikali Pius Hilla, Christopher
Msigwa na Grace Mwanga huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili wa
utetezi Peter Kibatala, Jonathan Mndeme, John Malya na Frederick
Kihwelo.
Wakati Mahakama inaendelea, washtakiwa Mbowe na wenzake
walikuwa wakionekana kwenye video ya ukumbini hapo lakini wao walikuwa
hawaoni kitu ndipo Mbowe akalalamika kuwa, kuwa haoni picha ya
mahakamani."Mheshimiwa hatuwaoni, tunawasikia sauti tu lakini
hatuwaoni," amedai Mbowe
Wakati marekebisho yakiendelea kufanyika
wakili Simba alishauri kuahirishwa kwa kesi iwapo mawasiliano
yatashindikana kutengemaa ushauri ambao ulikubaliwa na pande zote mbili.
Baada
ya dakika kadhaa za juhudi za wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano
kushindikana, washtakiwa waliulizwa kama wako tayari kuendelea kusomewa
mashtaka katika hali hiyo lakini Mbowe alikataa na hivyo pande hizo
mbili zikakubaliana kurudi mahakamani kesho, kwa makubaliano ya
washtakiwa wawepo mahakamani.
Nje ya mahakama kabla ya kuanza kwa
kesi, hali ya ulinzi iliimarishwa na kuonekana kuwa shwari bila vurugu
zozote ambapo wafuasi wa Chadema walionekana katika maeneo ya nje ya
mahakama wakitaka kuingia mahakamani hapo lakini wafuasi wachache
asilimia kubwa wakiwa ni viongozi ndiyo walipata nafasi ya kuingia ndani
ya ukumbi wa mahakama mtandao.
Hata hivyo baada ya kutoka nje ya
ukumbi huo baadhi ya wafuasi waliopata fursa ya kuingia ndani walianza
kuimba kuelekea getini wimbo uliosikika kwa maneno 'Mbowe siyo gaidi'
lakini askari walifanikiwa kuwanyamazisha huku wale walio nje wakijaribu
kuonesha mabango na kuimba wimbo huo hali iliyolazimisha askari wa
Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuwakamata baadhi ya wafuasi hao.
Mbali
na Mbowe washtakiwa wengine ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed
Lingwenya.Katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu,
washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi 2020 katika
hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na katika
maeneo mengine ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha kwa pamoja.
Na
wengine ambao hawakuwepo mahakamani kwa makusudi walitengeneza mikakati
ya kigaidi ambayo ni kufanya milipuko katika vituo vya mafuta na
mikutano ya hadhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba,
uchumi na sifa ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania
Shtaka la pili
la kufadhili vitendo vya ugaidi imedaiwa, katika siku na mahali hapo
Mbowe Mbowe aliwasaidia washtakiwa hao kutekeleza mpango wa kigaidi.
Pia
washtakiwa, Hassan, Kasekwa na Lingwenya wanadaiwa katika tarehe na
maeneo hayo washtakiwa hao watatu walipokea msaada kutoka kwa Mbowe kwa
ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi ambavyo ni kulipua vituo vya
mafuta na mikutano ya hadhara.
Aidha mshtakiwa Kasekwa anadaiwa
Agosti 5, 2020 katika eneo la Rau Madukani alikutwa na silaha aina ya
pistol yenye namba A 5340 aina ya Luger na risasi tatu bila ya kuwa na
kibali.
Katika shtaka la tano mshtakiwa Hassan anadaiwa Agosti
10, 2020 katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, kwa lengo la
kuhatarisha usalama wa nchi alitumia sare za jeshi la wananchi JWTZ na
Jeshi la kujenga Taifa JKT.
Sare hizo zilkuwa ni suruali moja ya
JKT, suruali nne, fulana moja, Koti la mvua moja, jacket moja, kofia
tano, overall tano, begi la kubebea vifaa vya lijulikanalo kwa jina la
ponjoo, vyeo vinne vya koplo, mikanda minne, soksi pea moja, sweta,
beji ya mafunzo ya parachuti, kibuyu cha kunywea maji vyote vikiwa
ni mali ya JWTZ pamoja na kisu aina ya AK 47 CCCP.
Post A Comment: