Katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 135 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 10,806 kwa ajili ya shule za msingi.
Hayo yameelezwa leo Julai 6,2021 na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu wakati akitoa kuhusu Mafanikio ya siku 100 za Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan na Mwelekeo wa utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 leo Julai 6,2021 jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 23.14 ni kutoka ruzuku ya Serikali Kuu maboma 1,852.
Aidha, kiasi cha Shilingi bilioni 18.17 kupitia Mapato ya Ndani ya Halmashauri zitatumika kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,455 ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi.
Vilevile amesema kupitia nyongeza ya fedha itakayopatikana kutoka kwenye tozo mpya za mitandao ya simu, OR TAMISEMI imetenga jumla ya Shilingi bilioni 93.73 kwa ajili ya kukamilisha maboma 7,499 ya vyumba vya madarasa (kutokana na mgao wa vyumba vya madarasa 10,000) katika mwaka 2021/22.
“Tumetenga jumla ya Shilingi bilioni 54.26 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,341 kwa ajili ya shule za Sekondari ambapo Shilingi bilioni 23.00 ni kupitia Bajeti ya OR TAMISEMI iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,840 vya madarasa katika Shule za Sekondari,”amesema.
Aidha, kupitia fedha zitakazopatikana kutoka tozo mpya ya mitandao ya simu, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 31.26 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 2,501 ya vyumba vya madarasa ya sekondari (kutokana na mgao wa vyumba vya madarasa 10,000)
“Tozo za mitandao ya simu itawezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 10,000 katika shule za msingi na sekondari,”amesema.
Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaandaa mwongozo ambao utakuwa na vigezo jinsi wananchi watakavyoshiriki kwenye ujenzi wa maboma ya elimu katika shule za msingi na sekondari.
“Ukamilishaji wa maboma ya Maabara za Masomo ya Sayansi
Zimetengwa Shilingi bilioni 26.07 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,043 ya vyumba vya maabara za sayansi,”amesema
Amesema mwaka 2020/21 jumla ya shilingi bilioni 28.99 zilitengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma 2,088 ya vyumba vya madarasa katika shule za Msingi.
Vilevile amesema zimetengwa jumla ya Shilingi bilioni 180.00 kwa ajili ya ujenzi wa Shule 300 za Sekondari katika Kata ambazo hazina Shule za Sekondari na katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi ambapo kila shule tumeitengea kiasi cha shilingi milioni 600 kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Amesema katika mwaka 2021/22 Serikali imetenga Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kuanza ujenzi awamu ya kwanza ambapo jumla ya Shule 10 za Sekondari za Wasichana hususan masomo ya sayansi kati 26 zitajengwa kwenye kanda 10.
Amezitaja kanda hizo pamoja na ya Magharibi, Nyanda za Juu, Mashariki, Dar es Salaam, Ziwa,Ziwa Magharibi, Kusini,Kati, Kanda Juu Kusini na Kaskazini Mashariki.
“Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bila kikwazo Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 312.05, ambapo Shilingi bilioni 142.77 zimetengwa kwa ajili ya Shule za Msingi na Shilingi bilioni 169.33 zimetengwa kwa ajili ya Shule za Sekondari,”amesema.
Vilevile, amesema jumla ya shilingi bilioni 38.15 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati 756 , kati ya fedha hizi Shilingi bilioni 28.20 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 559.
Amesema kila Jimbo la Tanzania bara litapata wastani wa Zahanati 3 na Shilingi bilioni 9.95 kutokana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya Zahanati 199.
“Katika kuboresha Afya ya Msingi Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 60.5 kwa ajili ya kujenga vituo vipya 121. Ambapo vituo vya afya 103 kupitia Mapato ya Ndani ya Halmashauri na vituo 18 vya afya kupitia ruzuku ya Serikali Kuu,”amesema.
Serikali imetenga Jumla ya Shilingi bilioni 55.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali 68 ambapo zilianza kujengwa mwaka wa fedha 2018/19.
Vilevile,Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 11.4 kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa Hospitali 31 .
Kwenye vifaa tiba,Waziri Ummy amesema Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 112.30 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo na kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambapo vitanunuliwa kwa pamoja na kugawiwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya (Vituo Afya na Hospitali za Halmashauri).
Vilevile,Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeidhinishiwa kusimamia Mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 144,429.77 baada ya kufanyiwa uhakiki kutoka barabara zenye urefu wa kilomita 108,946.19.
Amesema barabara za lami zilizopo ni kilomita 2250.69 (2.1%), barabara za changarwe ni kilomita 27,809.26 (25.6%) na barabara za udongo ni kilomita 78,886.25 (72.4%) na madaraja 3186 ambapo 29 ni makubwa na makalvati 69,020.
Pia,TARURA itaajiri wahandisi 200 kwa mikataba kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa kazi za barabara, ili wataalam wetu wapate uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kuhusiana na mafanikio ya siku 100 za Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Waziri Ummy amesema Serikali imepeleka kwenye Halmashauri 34 kiasi cha Shilingi bilioni 20.3 kwa ajili ya kuendelea na Ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 34 ambapo ujenzi unaendelea.
Aidha, Halmashauri 76 zimelekewa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 11 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati 3 kila Halmashauri.
“Kupitia mradi wa matokeo ya ufanisi (Result Based Financing -RBF) umefanyika uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya ambapo Zahanati 279, Vituo vya afya 46 na hospitali 22 za Wilaya zimepatiwa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 30.8 ili kuviwezesha vituo hivyo kufika ngazi ya nyota tatu katika ubora wa utoaji huduma,”amesema Waziri Ummy.
Aidha, kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya kiasi cha Shilingi 1.6 zimetolewa kwa ajili ya kununua vifaa tiba vya usingizi katika vituo vya afya 32 ili kuviwezesha vituo hivi kufanya upasuaji ikiwemo upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni.
Post A Comment: