WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema katika siku 100 za utawala wa Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kumekuwepo na mafanikio makubwa ya kiutendaji ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Waziri Mhagama aliyasema hayo leo Julai 5, 2021 alipotembelea banda la Ushirikiano linalotumiwa na mifuko hiyo kwenye maonesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba ili kujionea jinsi wanachama na wastaafu wanavyohudumiwa.
“Ninajisikia furaha kama Waziri ninayesimamia mifuko hii, katika siku hizi 100 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassa, kiasi cha shilingi bilioni 100 zimetolewa ili kuwalipa wastaafu na Mfuko unaendelea kulipa pensheni za kila mwezi kwa wakati na huku ukiendelea kulimaliza deni lililokuwepo wakati NSSF nayo ikifanya vizuri kwa kuongeza makusanyo ya michango ya wanachama inayofikia bilioni 100 kwa mwezi hivi sasa “ Alisema Mheshimiwa Waziri Mhagama.
Alisema serikali iliwaagiza watendaji wa mifuko yote miwili kufanya tathmini ya kiutendaji ili kutengeneza mfumo endelevu ambao hautatengeneza tena vurugu wala hautasumbua sekta kiujumla na kusumbua wastaafu.
“Nafurahi kuwaambia kwamba tathmini imeshafanyika na sasa wataalamu wanapitia ili kutoa matokeo ya hiyo tathmini na muda si mrefu kazi ikikamilika tutashirikiana na vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri ili kutoa tafsiri ya hiyo tathmini na hatimaye tupate ustawi wa sekta kwa ujumla.” Alifafanua Mhe. Waziri.
Mheshimiwa Waziri Mhagama alimsifu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba ambaye kwa kipindi kifupi tangu aanze kuuongoza Mfuko huo, Mfuko umeweza kufanya maajabu kwa kukusanya michango kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa mwezi.
Kwa upande wao, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba alisema, ushirikiano wao wa kutumia banda moja ili kutoa huduma, kumewarahisishia wanachama na wastaafu wa mifuko yote miwili kumesaidia kurahisisha utoaji huduma kwenye eneo moja na kwa urahisi.
“Toka mfuko uanze mwaka 2018 hadi Juni 30, 2021 jumla yawanufaika ( wastaafu) 144,000 wamelipwa mafao na tunalipa pensheni ya kila mwezi shilingi bilioni 58 kwa mwezi na tunalipa tarehe 25 ya kila mwezi na hatujawahi kuchelewa , hivyo tunakwenda vizuri napenda watanzania waelewe hivyo.” Alifafanua CPA Kashimba.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba yeye alisema ukuaji wa Mfuko umekuwa kwa kasi sana katika miaka michache iliyopita Mfuko ulikuwa na thamani ya Trilioni 3 lakini hadi kufikia tarehe 30 Juni kwamujibu wa hesabu ambazo bado hazijakaguliwa tayari kuna takriban Trilioni 5.2.
“Sisi tunazidi kumuahidi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tutahakikisha tunaweka nguvu kubwa ya kusajili wanachama kutoka sekta binafsi na ile isiyo rasmi informal sector, na ukuaji wa michango hiyo ni muelekeo sahihi wa kutimiza maagizo ya Mheshimiwa Rais.” Alibainisha.
Post A Comment: