Wananchi wa Kijiji cha Kituri, Kata ya Kileo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro, wameiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu katika mto Ghona unaounganisha vijiji vya Kifaru na Kileo ili kuepukana na majanga ya vifo vinavyotokea wakati wa kuvuka.
Ombi hilo limetolewa jana na wananchi mbele ya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ambayo ilitembelea draja hilo, kujionea adha waliyonayo wananchi hao wakiwemo wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Corman Shirima, alisema kutokana na mvua za masika kuvunja kingo za daraja na kupelekea kuharibika kwa miundombinu ya barabara na hivyo kusababisha adha kubwa kwa wananchi.
Alisema kutokana na adha hiyo ya daraja kuvunjika kingoza mto huo, wananchi wanalazimika kuzunguka hadi Kata ya Kifaru ni changamoto kwao.
Philemon Cheyo, mkazi wa kijiji cha kituri aliiomba serikali, iwasaidie kuwajengea daraja hilo kwa haraka kwa sababu ndiyo barabara kuu inayotumiwa na wanafunzi kwenda shuleni na kuwapeleka wagonjwa katika hospital ya Usangi na hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi.
Diwani wa kata hiyo, Salimu Zuberi, alisema mto huo una viumbe hatari wakiwemo mamba ambao ni hatari, hivyo akaiomba serikali kupitia Wakala wa barabara TANROADS kulimimina zege daraja hilo, kwani limesababisha vifo vya watu kadhaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi, Mazingira, Innocent Msemo alisema wameiona adha hiyo na kwamba watakapo kwenda kwenye vikao vyao watalipa kipaumbelea daraja hilo ili kuisukuma serikali iweze kulijenga kwa haraka daraja hilo.
Awali Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Salehe Mkwizu alisema wanaendelea kufanya mazungumza na Wakala wa Barabara (TANROADS), ili kulipa kipaumbelea kwa kulijenga daraja hilo kwani daraja hilo ni kiungo muhimu.
Post A Comment: