Na Mbaraka Kambona,
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Abdallah Ulega amewahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika
sekta za mifugo na uvuvi ili waweze kuzitumia kujikomboa kimaisha.
Ulega alisema hayo
alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo katika Monesho ya 45
ya biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu
Nyerere jijini Dar es Salaam Julai 5, 2021.
Akiwa katika maonesho hayo
alisema kuwa vijana watumie nafasi hiyo ya maonesho kwenda kujifunza fursa
mbalimbali za kibiashara na za uwekezaji zinazopatikana katika sekta za mifugo
na uvuvi kwa sababu wizara ya mifugo na uvuvi mambo yake mengi ni ya uzalishaji
na biashara.
“Kila kitu kilichopo katika
wizara hii ni fursa katika biashara na ni fursa ya uwekezaji, hivyo
tunawashauri vijana kutumia fursa hii ya maonesho kujifunza na kutumia elimu
watakayoipata kuboresha maisha yao huko wanakoishi,” alisema Ulega
Aliendelea kusema kuwa katika
banda la wizara hiyo kuna wataalam mbalimbali ambao wanatoa elimu na mafunzo
yanayohusu ufugaji, hivyo wakifika hapo watajifunza namna ya kufuga kuku, ng’ombe,
mbuzi au Samaki kibiashara.
Aliongeza kuwa kuna vijana
wengi wanaotafuta kazi lakini bado hawajafanikiwa, hivyo aliwashauri kwenda
kujifunza fursa kubwa za kibiashara zitakazowasaidia kujipatia ajira na kukuza
uchumi wa nchi pia.
“Serikali ya awamu ya sita
ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kufungua milango ya biashara,
kwa hivyo, hivi sasa wale wote wenye kiu ya kujifunza na kufanya kazi ya
uzalishaji tunawakaribisha hapa ili waweze kufanya kazi hiyo ambayo itakuwa na
manufaa sio kwao tu bali kwa taifa pia,’’aliongeza Ulega
Katika hatua nyingine, Waziri
Ulega amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ikiwemo Wakala ya Vyuo vya
Mafunzo ya Mifugo (LITA) na Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kubuni mafunzo yatakayojumuisha
watu wa elimu ya chini kabisa ambao wengi wao ni darasa la saba.
Alisema kwa sasa vijana wengi ambao hawajasoma wanakimbilia katika kuendesha bodaboda kwa maana ndio njia wanayoiona rahisi ya kujipatia kipato huku akizitaka taasisi hizo kuja na mkakati maalum wa kuanzisha mafunzo ya kuwafundisha vijana hao fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hizo mbili na wakazitumia kujiajiri na kufanya uzalishaji mkubwa utakaowezesha hata nchi kupata mapato.
Post A Comment: