Mwenyekiti
wa jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa
Njombe (UWT) Scolastika Kevela amevitaka baadhi ya vyama vya upinzani
kuacha kuleta chokochoko nchini kwa kigezo cha kutaka katiba mpya.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kevela ambaye pia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, amesema
Rais Samia Suluhu Hassan ameshatolea ufafanuzi suala hilo kwa kusema
kuwa apewe muda hivyo wanapaswa kutulia.
Amesema
kauli hiyo ya Samia ilipaswa kuheshimiwa na kupokelewa kwa mtazamo
chanya na wananchi wote hususani wale wanaoleta chokochoko hasa
wapinzani ambao muda mwingi wamekuwa wakianzisha na wakitafuta sababu za
kuanzisha chokochoko.
"Rais
Samia aachwe afanye kazi yake tuliyomtuma wananchi kwa mujibu wa
katiba, ndiyo kwanza uongozi wake una miezi minne madarakani, hizi
kelele za wanaotaka katiba zinatolewa kwa lengo la kutaka kumtoa katika
reli ya kuwatumikia watanzania." Amesema Scolastika.
Aidha
amesema anashangazwa na wapiga kelele hao kuanza kujitokeza kwa wingi
na kuleta chokochoko hizo ndani kipindi hilo kifupi cha uongozi wa Rais
Samia tofauti na hali ilivyokuwa kabla yake ambapo kulikuwa na kiongozi
mwingine katika nafasi hiyo lakini hawakuthubutu kufanya hivyo.
"Mimi
kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe nalaani chokochoko hizo na zaidi
nawaomba watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hii kuendelea kuunga
mkono juhudi anazozifanya Rais wetu kutuletea maendeleo watanzania
wote." Amesema Scolastika.
Katika
hatua nyingine Mwenyekiti huyo amempongeza Rais Samia kwa juhudi
mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuimarisha mahusiano ya
kidiplomasia na mataifa mengine duniani
Amesema
kitendo cha Rais huyo kukutana na viongozi kutoka mataifa mbalimbali na
wakati mwingine kufanya ziara katika mataifa hayo, kunaonyesha dhamira
yake ya kushirikiana na mataifa hayo katika masuala mbalimbali ikiwemo
ya ujenzi wa uchumi imara wa taifa.
Post A Comment: