Afisa Miradi wa Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi, Annamaria Mashaka, akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA)  wa Kata ya Msange wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jana Halmashauri ya Wilaya ya Singida.


 Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui, akizungumza katika mafunzo hayo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe akizungumza katika mafunzo hayo/
Mafunzo yakiendelea.
Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Hassan  Ipande akizungumza katika mafunzo hayo/
Mjumbe wa Kamati hiyo Felister John akizungumza kwenye mafunzo hayo/
Mjumbe wa Kamati hiyo Theresia Yambi akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
  

 

Na Dotto Mwaibale,Singida.

 

SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi limewakutanisha kwa pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya Kata kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.

Wajumbe hao ambao ni viongozi kutoka idara mbalimbali za serikali, Asasi za Kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu chini ya mwenyekiti wake Afisa Mtendaji wa Kata wamekutana juzi kwenye kikao cha mafunzo ya kuwajengea uwezo na kujadili mbinu za  kukabiliana na ukatili Kata ya Msange katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. 

Akizungumza katika kikao hicho Afisa Miradi wa Shirika hilo Annamaria Mashaka alisema baada ya kuzijengea uwezo kamati za Mtakuwwa ngazi ya kata wanaamini zitakwenda kutekeleza mpango huo kupitia majukumu yaliyoainishwa na mwongozo ambayo yamewekwa pia katika lugha rahisi na kamati hiyo ili waendelee na mchakato wa kutokomeza ukatili kwa jamii ya watu wa Msange.

Alisema lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hiyo ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na mtoto ambao katika halmashauri hiyo unafanyika katika Kata za Msange, Ikhanoda, Mudida na Mukuro.

" Miongoni mwa majukumu waliojipangia kama kamati katika utekelezaji wa mpango huo ni kuendelea kutoa elimu, kuhamasisha jamii kuepukana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto," alisema Mashaka.

Aidha Mashaka alisema kamati hiyo ineelekeza nguvu katika kuibua changamoto hama matukio yote yanayotokana na ukatili na si tu kuyaibua na kufanya ufuatiliaji ili haki iweze kupatikana kwa wahanga wa ukatili na watuhumiwa waweze kuhukumiwa kutokana na vitendo wanavyofanya. 

Pia Mashaka alisema sambamba na kutoa elimu na kuibua matukio kamati hiyo imewekeza nguvu katika kuhamasisha jamii kupitia mbinu mbalimbali yakiwemo mabonanza ambayo yatafanywa kwa kushirikiana na Polisi Jamii ngazi ya kata yakiwa na lengo la kutokomeza ukatili huo katika kata hiyo ya Msange.

  Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui alisema wamekutana na kamati hiyo kuongelea ukati huo na aina tano ambazo zinawakumba sana wanawake na watoto wadogo ambao ni ukatili wa kingono, kimwili, kisaikolojia, kiuchumi na ukatili wa kiafya.

Alisema wanakamati hao pia walitamani kujua je mtu akifanyiwa ukatili sehemu husika ya kwenda kutoa taarifa ni wapi ambapo pia walipitia vipengere mbalimbali ili kujua ni sehemu gani wataweza kulisema suala hilo la ukatili.

Alisema katika kata hiyo  bado kunaonesha  kuna ukatili wa ukeketaji ambao ni wa kiafya, kimwili na kingono ambao unafanyika kwa siri kubwa sana ambapo wamegundua mbinu mpya kwa kufanya ukeketaji kwa mtoto mdogo kuanzia anapozaliwa mpaka anapokuwa na miaka mtano.

Alisema ukatili huo wanaufanya kwa kutumia chumvi ya magadi, mazinzi yanayotoka juu kwenye nyumba za tembe na kusugua sehemu za siri kwa kutumia mtula ambapo pia mabibi wanafuga kucha ambazo hutumika kumfinya mtoto kwenye kiungo chake ili kumkeketa jambo ambalo wamekiri kuwa ni baya. 

Kamati hiyo imepanga mkakati wa muda wa miezi mitatu ili kuendelea kutoa elimu kuhusu ukatili huo na kuwa wataitoa makanisani, misikitini, mashuleni, kwenye masoko, sehemu hatarishi na kwenye mikusanyiko ya watu.

Mjumbe wa Kamati hiyo PC Christian kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Msange alisema matukio hayo ya ukatili ni muhimu yakatokomezwa na changamoto kubwa iliyopo ni wahusika wa matukio hayo kushindwa kufika kwenye vyombo vinavyotoa haki kutoa ushahidi jambo linalosabisha kesi hizo kuishia njiani bila kutotolewa hukumu.

Share To:

Post A Comment: