Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdullah amekipongeza Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha kinatoa wahitimu wenye uzalendo, weledi na uadilifu katika Uongozi.
Makamu huyo wa pili wa Rais ametoa kauli hiyo wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi wa Chuo hicho kwa Kampasi ya Karume Zanzibar ambayo yameanza kujengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya chuo hicho.
Mhe.Hemed Suleiman Abdullah amesema kuwa Chuo kinatoa wahitimu waliobobea katika fani zao na wenye weledi katika masuala ya uongozi, maadili na utawala bora kitu ambacho kinaongeza tija katika Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Makamu huyo wa pili wa Rais amewasisitiza wadau wa Maendeleo kuchangia ujenzi wa Mabweni hayo ya wanafunzi kwani kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kutatua changamoto ya malazi kwa wanafunzi 1536 chuoni hapo.
“Nampongeza Mbunge wa Jimbo la Mpendae kwa niaba ya Turky Foundation amechangia jumla ya Shilingi Millioni Ishirini (20,000,000/=) ikiwa ni jitihada katika kuchangia uboreshaji wa Elimu hapa Zanzibar, hivyo natoa wito kwa wadau wa Maendeleo waliopo Zanzibar kujitokeza kusaidia kufanikisha mradi huu utakao gharimu shilingi bilioni 15.2.” Alisisitiza Kiongozi huyo.
Pia Makamu wa Pili wa Rais amemtaka mkandarasi wa mradi huo SUMA JKT kuhakikishakukamilisha mradi kwa wakati na kwa ufanisi.
Akizungumzia suala la uvamizi wa eneo la chuo na wauzaji wa madagaa Makamu huyo wa pili ameahidi kuwa suala hilo litamalizwa ndani ya kipindi kifupi kijacho hivyo chuo kiendelee kuwa na uvumilivu katika hilo .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Mhe.Stephen Wasira amesema chuo kimeendeleza dhima ya kuanzishwa wake kwa kuwa kitovu cha kutoa Elimu ya Uongozi ,Uzalendo, Maadili na Utawala bora.
Akizungumza na hadhira katika hafla hiyo Mkuu wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila ameishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kukisaidia Chuo katika ukuaji wake na kutatua Changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikikabili Chuo hicho.
Makamu wa Pili wa Rais ameweka jiwe la msingi la mabweni chuoni hapo kwa niaba ya Mhe.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere –Kampasi ya Karume
Zanzibar
26/07/ 2021.
Post A Comment: