Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Stephen Adili akimkabidhi zawadi ya gari mshindi wa kampeni ya SimBanking “Mzigo Promosheni,” Kevin Ngao katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha CRDB Wakala (wapili kushoto), Ericky Willy na Meneja Biashara Kanda ya Mashariki, George Yatera.
Dar es Salaam Tanzania, July 7, 2021 – Benki ya CRDB imekabidhi gari aina ya Toyota IST kwa mshindi wa kwanza wa kampeni ya “SimBanking Mzigo Promosheni,” anayejulikana kwa jina la Kelvin Ngao. Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Stephen Adili alisema mshindi huyo amepatikana kwa kufanya miamala mingi zaidi kupitia huduma ya SimBanking.

“Kampeni yetu inalenga katika kuwahamasisha wateja kujenga utamaduni wa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwamo SimBanking kufanya miamala yao. Tumekuwa tukitoa zawadi ya Sh. 100,000 kwa wateja wetu wenye miamala mingi zaidi kila siku na leo hii tunakwenda kutoa zawadi ya gari kwa mshindi wa jumla wa mwezi Juni, Kevin Ngao,” alisema Adili.

Adili aliongezea kuwa katika kampeni hiyo Benki ya CRDB pia inatoa elimu kwa wateja wake juu ya matumizi ya huduma ya SimBanking ambapo pia wateja wamekuwa wakiulizwa maswali kupitia mitandao ya kijamii na radio na kujishindia zawadi ya Sh. 30,000. Mpaka sasa tayari benki hiyo imeshatoa jumla ya shilingi milioni 15 kwa washindi 500.
Akielezea mafanikio ya kampeni hiyo alisema katika kipindi cha mwezi Juni matumizi ya huduma ya SimBanking yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 kutokana na uelewa wa wateja juu ya urahisi na unafuu wa SimBanking katika kupata huduma. 

Adili alisema kampeni hiyo pia imezaa matunda katika upande wa elimu ya kufungua akaunti kupitia SimBanking App ambapo hadi sasa zaidi ya wateja 30,000 wameshafungua akaunti kupitia mfumo huo wa kidijitali.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi wa shindano hilo Kevin Ngao aliishukuru Benki ya CRDB kwa zawadi hiyo ya gari huku akibainisha siri ya ushindi ni kujenga utamaduni wa kutumia SimBanking kufanya miamala yake. 
“Ninafurahia sana kufanya miamala kupitia SimBanking iliyoboreshwa, imekuwa rahisi na nafuu sana kutumia. Sasa hivi miamala yangu yote nakamilisha kupitia SimBanking, iwe kufanya malipo kupitia CRDB Lipa Namba, kutuma pesa, kulipia bima, kulipia kodi na kutoa fedha kwa CRDB Wakala/ ATMs na Tawini bila ya kadi,” alibainisha Kevin.

Akihitimisha hafla hiyo Meneja wa Biashara Kanda ya Mashariki Benki ya CRDB, George Yatera alimpongeza mshindi huyo pamoja na washindi wengine wote ambao wamepata zawadi kupitia kampeni hiyo huku akitoa rai kwa wateja wengine wa benki hiyo kushiriki kampeni kwa kuendelea kufanya miamala kupitia SimBanking.

“Kampeni yetu bado ina miezi miwili zaidi hadi mwezi Agosti, zawadi bado ni nyingi hivyo nitoe rai kwa wateja wetu kuendelea kufanya miamala kwa wingi Zaidi lakini pia kufuatilia mitandao yetu ya kijamii ambapo pia tunatoa zawadi,” alihitimisha Yatera. 


Share To:

Post A Comment: