Wananchi wa Kijiji cha Itamka wakiwa wameubeba mwili wa Bakari Hassani kwa ajili ya kufanya taratibu za mazishi baada ya kukabidhiwa na Serikali.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF) Ivo Ombella, akiwatizama kwa kamera maalumu askari wa jeshi hilo walipokuwa katikati ya bwawa hilo wakiitafuta miili hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Eliya Digha akizungumza na wananchi wakati ndugu wa Bakari Hassan wakikabidhiwa mwili wa kijana wao baada ya kupatikana.
Na Dotto Mwaibale, Singida
JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa limefanikiwa kuitoa kwenye maji miili yote ya watu watano walio kufa maji kwenye Bwawa la Ntambuko Tarafa ya Ilongero mkoani hapa kufuatia mtumbwi waliokuwa wamepanda kupigwa na wimbi na kupinduka na kusababisha watu hao kupotelea kwenye maji.
Kwa takribani siku mbili mfululizo kuanzia juzi mpaka jana kikosi maalumu cha askari wa Jeshi la Zimamoto kutoka mikoa mitano kimefanikiwa kuopoa maiti hizo zilizozama kwenye bwawa hilo.
Miili ya marehemu iliyofanikiwa kutolewa kwenye maji imetambuliwa kwa majina ya Bakari Hassan (25), Abubakary Hamis (35), Hamis Ally (38) Ally Hamis (18) ambaye ni Mwanafunzi wa Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Mrama na Ayoub Mohamed (39) wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Itimka, Ilongero mkoani hapa.
Kazi hiyo ya kuitafuta miili hiyo ilifanywa na Kikosi cha Jeshi la Zima Moto na Ukoaji kutoka mikoa ya Manyara, Singida Mwanza, Dodoma na Shinyanga kwa kushirikiana na wenzao wa Singida na wananchi.
"Kazi inaendelea lakini naamini huenda zoezi likawa gumu kutokana na askari kukosa vifaa vya kisasa. Kama unavyoona askari wameazima mitumbwi miwili na nyavu za wavuvi wenyeji wa hapa kufanyia shughuli zao ambapo toka jana asubuhi litokee tukio hilo hadi leo 'jana asubuhi ni mwili mmoja tu wa Bakari Hassan ndio ulikuwa umepatikana," alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Salum Masimba kabla ya kupatikana kwa miili hiyo yote.
Hata hivyo Masimba ameiomba Serikali kulisaidia jeshi hilo kwa kuwapatia dhana za kisasa kwa ajili ya masuala ya uokozi hapa nchini.
Alisema tangu juzi kikosi hicho kilipowasili kwa kazi hiyo maalumu hawakuonekana kuwa na vifaa vyovyote zaidi ya nguo za kuogelea na mipira ya kuvaa kwa ajili ya kujizuia kuzama.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na uokoaji mkoani Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF) Ivo Ombella aliwahakikishia wananchi kuwa miili yote itapatikana kwani vijana wake walikuwawamejipanga vizuri kwa kazi hiyo.
"Vijana hawa wana weledi mkubwa na kazi hii na wanaendelea vizuri, na hatutaondoka eneo la tukio mpaka mili yote iliyosalia ipatikane," alisema Ombella.
Huku Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge akikisihi kikosi cha uokoaji kutumia utaalamu wao wote kuhakikisha wanarudisha faraja kwa wote waliopoteza ndugu zao.
"Umati huu una hamu kubwa ya kuwaona wapendwa wao wote waliopotea kwenye maji kupitia tukio hili, mwanzo walikuwa saba lakini wawili walifanikiwa kuokolewa wakiwa hai ni matarajio yangu kuona miili yote inapatikana na kukabidhiwa ndugu zao ili mazishi ya heshima yafanyike" alisema Mahenge kabla ya kupatikana kwa miili hiyo yote.
Post A Comment: