Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni
(Mb) akiiagiza Menejimenti ya Benki ya TIB kukusanya madeni na mikopo
yote iliyotolewa mwaka 2016 bila kufuata taratibu, alipofanya ziara
katika Benki hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo (katikati)
akieleza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) alipofanya ziara katika
Taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki hiyo, Bw. Charles Singili.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili, akieleza kuhusu
utekelezaji wa majukumu ya Benki yake, wakati wa ziara ya Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo
pichani) katika Taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb)
akiongoza Mkutano wa Menejimenti ya Benki ya TIB, alipofanya ziara
katika Taasisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa kutembelea taasisi
zilizochini ya Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb)
(katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Charles Singili, wakiwa katika
picha ya pamoja na Viongozi wa Menejimenti ya Benki ya TIB, jijini Dar
es Salaam.
(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango, Dar es Salaam)
************************************
Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza
Benki ya TIB kuhakikisha madeni na fedha zote za mikopo zaidi ya
shilingi bilioni 535.3 zilizokopeshwa kwa wateja wao bila kufuata
taratibu pamoja na wadaiwa sugu zinarejeshwa ili zitumike kutoa mikopo
kwenye maeneo mengine yenye tija.
Mhandisi Masauni ametoa maagizo
hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea Benki ya TIB ambapo alikutana
na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Benki hiyo na wafanyakazi,
katika mwendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
“Kwa njia
yeyote ile ni lazima fedha za wananchi zirejeshwe hivyo nawaagiza pia
kuleta mapendekezo Serikalini ili kuangalia iwapo kuna eneo ambalo
Serikali inaweza kuingilia kati kuhakikisha tunaokoa fedha za wananchi
zilizowekezwa katika miradi isiyo na tija”, alieleza Mhandisi Masauni.
Alisema
kuwa nchi inapoelekea inahitaji kuona Benki ya TIB inashiriki
kikamilifu katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa kwa
kuiwezesha Serikali kukopa katika taasisi za fedha za ndani badala ya
kukopa kutoka benki za nje na kuwataka watendaji wa benki hiyo kusimamia
ipasavyo Benki ili jambo hilo liwezekane.
Aidha Mhandisi Masauni
ameitaka Benki hiyo ihakikishe mikopo yote inayotolewa iwe na tija ili
kuepuka mikopo chechefu na kufadhili miradi inayoweza kuisababishia
hasara Benki hiyo na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya TIB, Bi. Mary Mashingo, alisema kuwa
taasisi hiyo inashauku ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi
mikubwa ya kimkakati inayoendelea nchini na kusaidia katika kutekeleza
Sera katika sekta mbalimbali za maendeleo hivyo itashirikiana na
Serikali kubuni mbinu za kuzirejesha fedha zilizokopeshwa kabla ya mwaka
2016 na pia kupunguza riba kwa kuwatumia wataalam mbalimbali.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Bw. Charles Singili, alisema kuwa
Benki yake kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Wizara ya Fedha na
Mipango wanafanya jitihada ya kuhakikisha fedha hizo, zikiwemo shilingi
bilioni 168 ambazo kesi zake ziko mahakamani na kiasi kingine cha
shilingi bilioni 368 zilizoko mikononi mwa wadaiwa sugu zinarejeshwa ili
zitumike kutoa mikopo kwa wawekezaji wengine ili kuchochea upatikanaji
wa ajira na pia kodi ya Serikali kupitia miradi hiyo.
Vilevile
alieleza kuwa namna pekee itakayoongeza wigo wa kodi ni uwepo wa miradi
mingi inayozalisha, na kumhakikishia Mhe. Masauni kwamba Benki yake
itazifuatilia fedha hizo ili ziboreshe mizania ya mtaji ya Benki hiyo na
kuziwekeza katika meneo yatakayosaidia kujibu matatizo ambayo nchi
inakabiliana nayo na kuboresha maisha ya wananchi.
Home
Unlabelled
MHANDISI MASAUNI AAGIZA MIKOPO NA MADENI YA BENKI YA TIB KUREJESHWA
Post A Comment: