Na Juma Mizungu,
Meya Jiji la Dar es salaam Mhe Omary Kumbilamoto ametoa Semina fupi ya namna gani vikundi ambavyo vinapata mikopo ya Halmashauri ya Jiji kuitumia mikopo hiyo ili ikawanufaishe kiuchumi. Semina hiyo imejumuisha vikundi mbalimbali vya vikoba ambavyo vinatoka katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam.
Mhe. Kumbilamoto amevitaka vikundi vyote ambavyo vinapata mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji kuwa na malengo mapana katika kuzitumia fedha hizo kwani changamoto kubwa iliyokuwepo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Wajasiriliamali wengi hawaitumii mikopo katika kuzalisha wengi wao hugawana fedha hizo na hatimaye kushindwa kufanya marejesho.
Mhe. Kumbilamoto aliendelea kwa kutoa wito kwa Wajasiriliamali wote pamoja na vikundi vyote vya Vijana, wakinamama pamoja Walemavu waliopata mikopo wanapaswa kufanya marejesho ili kuwapa fursa Wajasiriliamali wengine kukopa.
"Changamoto kubwa tuliyo nayo ni marejesho Vikundi vingi vimepata mikopo ila tatizo kubwa hawafanyi marejsho nitoe wito kwa vikundi vyote kufanya marejesho ili kuwapa fursa na wengine kukopa" alisema Mhe Kumbilamoto
Aidha Mhe. Kumbilamoto alivipongeza vikundi vya Sedo kwa kuendelea kuvilea vikundi vidogo vidogo pamoja na kikundi cha furaha kwani ni vikundi vya mfano na vimeweza kutoa ajira kwa watu wengi kupitia fedha walizo kopeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam.
Mwisho Mhe Kumbilamoto alizungumza kwa njia ya Simu na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ludigija kuhusiana na vikundi vyenye miradi mikubwa ambavyo tayari vipo katika hatua ya kupata mikopo mikubwa, Mhe. Ludigija aliwapongeza Wajasiriliamali wote pamoja na Vikundi vyote vya Vikoba na kuwataka kuendelea kuitumia vyema Mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji ili iwanufaishe kiuchumi.
Post A Comment: