KATIBU Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo akizungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar katika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kisiwandui.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa CCM katika Kikao cha Wazee wa CCM, kilichofanyika Kisiwandui.
BAADHI ya Wazee wa Chama Cha Mapinduzi wakiwa katika kikao hicho cha Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo, amesema Chama kitaendelea
kuenzi,kulinda na kuheshimu kundi la wazee kwani ndiyo chimbuko la
maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa ndani ya Chama.
Hayo ameyasema
leo katika mwendelezo wa ziara yake visiwani Zanzibar wakati alipokutana
na Wazee wa Baraza la Wazee Zanzibar pamoja na wawakilishi wa wazee
kutoka katika Wilaya zote za chama cha mapinduzi.
Chongolo,
amesema ziara yake hiyo ni ya kujitambulisha tangia ateuliwe kushika
nafasi hiyo hivyo amefarijika kukutana na wazee hao kwa lengo la
kusikiliza ushauri,maoni na mapendekezo yao ili yaweze kumsaidia katika
utekelezaji wa majukumu yake.
Alifafanua kwamba mafanikio
yaliyopo hivi sasa ndani ya chama yameasisiwa na wazee hao ambao
walifanya kazi kubwa ya kuanzisha taasisi imara ya kisiasa ambayo ni CCM
inayotokana na vyama viwili vya ASP na TANU.
‘’Wazee wetu enzi
za ujana wenu mlianzisha chama hiki tena kwa kujitolea na mkatuwekea
misingi na taratibu imara zinazosababisha leo hii CCM inaheshimika
kutokana na nguzo muhimu za kiuongozi,kiutawala na kisiasa mliyoiweka
nyinyi’’ alisema Katibu Mkuu huyo Chongolo.
Katika maelezo yake
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba kupitia kitabu cha taratibu za sehemu
ya wazee wa CCM toleo la Juni 2019, kimeeleza mambo mbalimbali
yakiwemo kurithisha kwa Taifa busara,hekima na ujasiri wao ndani ya
jamii.
Alisema pia wana jukumu la kuendelea kuwa mfano bora wa
tabia njema kwa Taifa na hivyo kuongoza mafanikio, imani,malengo na
madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi.
Katibu mkuu huyo, alisema pia
wazee wana jukumu la kushauri viongozi wa Chama kwa hekima kuhusu njia
bora za ujenzi wa CCM na Taifa.
Aliendelea kufafanua kwamba wazee
hao wanatakiwa kuona nchi inaendeshwa kwa misingi ya kudumisha
Amani,utulivu,Demokrasia na Uongozi bora.
Pamoja na hayo alisema
wanatakiwa kuhifadhi, kukuza na kudumisha Umoja na uzalendo wa Kitaifa
pamoja na kuwaunganisha Wazee wote wa CCM katika imani na mwelekeo wa
kiitikadi wa Chama.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.
Abdulla Juma Mabodi, amesema Wazee hao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya
kushauri masuala mbalimbali yenye tija ndani ya Chama na Serikali kwa
ujumla.
Alisema ushindi wa CCM katika Chaguzi mbalimbali za Dola
na ndogo za majimbo zimetokana na miongozo inayotolewa na Wazee hao
kwani wana uzoefu na uwezo mkubwa katika masuala ya kisiasa,kiuchumi na
kijamii.
Mapema akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la
Wazee wa CCM Khadija Jabir, alisema wazee hao wapo imara na wanaendelea
kushiriki masuala mbalimbali ya Chama Cha Mapinduzi.
Kupitia
kikao hicho Mwenyekiti huyo aliahidi kwamba wataendelea kushauri
viongozi mambo mbalimbali yatakayoongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji na
kiuongozi.
Ziara hiyo ya siku mbili ilianza Julai 4 na
kuhitimishwa Julai 5,2021 alipokutana na wazee wa CCM,Watumishi wa Chama
pamoja na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.
Hussein Ali Mwinyi.
Post A Comment: