Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipofanya ziara katika hospitali hiyo kuangalia utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu alilolitoa baada ya kuapishwa mapema mwaka huu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hospitali zisizuie miili ya marehemu.
Dkt. Gwajima amewataka wananchi kufuata taratibu za kuchukua miili ya marehemu kwa mfano kuwa na vielelezo vinavyotakiwa kwani wengi wamekuwa wakienda vyumba vya kuifadhi miili bila kuwa na vielelezo.
Amesema baadhi ya kero na malalamiko ambayo amekuwa akipelekewa yanatokana na baadhi ya wananchi au ndugu wa wagonjwa kutofuata mifumo na taratibu za kuchukua miili ya marehemu kwenye vyumba vya kuiifadhi.
“Nimegundua baadhi ya ndugu wa marehemu wanatoka wodini na kwenda katika vyumba vya kuhifadhi miili bila kuwa na vielelezo stahiki, hivyo nawaomba ndugu kutoa ushirikiano ili miili ichukuliwe kwa wakati.” Amefafanua Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima.
Katika ziara hiyo pia ameagiza uongozi wa hospitali zote nchini kushughulikia kero haraka ili ndugu wa wagonjwa waendelee na shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri ameagiza uongozi wa hospitali kufuatilia wagonjwa wasio na uwezo wa kulipia matibabu ambao wamekuwa wakienda kwa viongozi wa Serikali za mitaa kupatiwa barua ili kutibiwa kwa msamaha huku baadhi ya barua hizo zikionekana hazina uhalisia. Amesema tabia hiyo inawanyima wananchi halisi wenye kuhitaji huduma ya msamaha na hii siyo haki na ikibainika hatua zitachukuliwa.
“Ukifuatilia katikati ya mifumo yetu, utabaini matapeli wameingilia mifumo na baadhi ya wanaohudumiwa wanakuwa siyo walengwa. Sasa ninaiagiza hospitali kufanya uchunguzi wa barua zilizoletwa hapa Muhimbili na tukibaini barua hizo ni za kugushi, fedha zote zilizotumika kuwahudumia wagonjwa ambao si wa msamaha, wahusika walioandika barua za kuwa wale wasamehewe watapaswa kulipa fedha zote na kuchukuliwa hatua stahiki.” Amesema Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima
Post A Comment: