Baraza la madiwani halmashauri ya Wilaya ya Busega limetaka uwepo wa
Mahakama ya Wilaya Busega. Hayo yamesemwa na wajumbe wa baraza hilo
wakati wa kikao cha baraza la madiwani robo ya tatu lililofanyika tarehe
04 Juni 2021 ukumbi wa Silisos.
Diwani kata ya Nyasimo Mhe.
Mickness Mahela amehoji kuhusu suala la uwepo wa Mahakama wilayani
Busega, akisema kwamba imekuwa kero kubwa kwa wakazi wa Busega
wanapotaka kupata huduma ya mahakama, kwani inawalazimu kwenda Wilaya
jirani ya Bariadi kupata huduma hiyo.
“Wilaya ya Busega ina
takribani miaka tisa kwasasa, hivyo uwepo wa mahakama ni muhimu kwa
wananchi wetu” aliongeza Mhe. Bi. Mickness Mahela. Wajumbe wa baraza
hilo wamekiri kwamba uwepo wa mahakama ni suala lisilopingika, huku
wakidai kwamba wilaya inahitaji mahakama ili kuondoa kero ya wakazi na
wananchi wa Busega.
Akitoa ufafanuzi wa suala la uwepo wa
mahakama wilayani Busega, mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya
Busega Bw. David Pallangyo anasema kwamba ni suala ambalo Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya imekua ikifuatilia kwa ukaribu na inaendelea na ufutiliaji.
Kwa upande mwingine ameeleza kwamba licha ya watumishi wa mahakama
kupangiwa kufanyia kazi zao wakiwa Busega lakini bado wanafanyia kazi
zao wilayani Bariadi.
Aidha, hoja ya matengenezo ya magari
iliibuliwa na wajumbe huku wakitaka uwepo wa gereji ya halmasuri ili
kuwa na ufanisi wa matengenezo ya magari hayo kuliko kupeleka magari
hayo kwa Wakala wa Ufundi wa Umeme na utengenezaji wa Magari ya Serikali
(TEMESA). Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Mkurugenzi Mtendaji Bw.
Anderson Kabuko licha ya changamoto ya TEMESA, lakini tayari marekebisho
na matengenezo madogo yanafanyika kwa baadhi ya magari na kazi hiyo
inafanywa na fundi wa halmashauri.
Suala la stendi ya Wilaya
ambayo imeanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu, pia
limepata wasaa wa kujadiliwa na baraza hilo. Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema tayari
halmashauri imevunja mkataba na mkandarasi wa awali ambae alikuwa
akijenga stendi hiyo kutokana na kutofikia ubora wa ujenzi, na tayari
utaratibu unafanyika ili kumpata mkandarasi mwingine. Baraza hilo
limetaka ujenzi wa wa stendi hiyo uboreshwe hasa njia za kupita magari
ili kuondoa usumbufu na kero.
Akiahirisha kikao cha baraza hilo,
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe, ametaka
kuendelea kwa juhudi ujenzi wa stendi ya Wilaya, na kuagiza kwamba
kwasasa hatuhitaji mkandarasi, mhandisi wa ujenzi kwa kushirikiana na
Meneja wa TARURA kufanya kazi ya ujenzi kuendelea na ujenzi wa stendi ya
Wilaya, Nyashimo. Kwa upande mwingine ameomba viongozi wa mkoa
kufuatilia suala la mahakama ili wilaya ya Busega iweze kupata mahakama.

Post A Comment: