Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka akizungumza kumkaribisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipotembelea taasisi iliyo chini ya wizara yake ya (Tantrade).

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) alipotembelea taasisi hiyo.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) akizunguka katika mabanda mbalimbali kukagua matayarisho ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajia kuanza tarehe 28 Juni, hadi 13 Julai, 2021 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

....................................................................................

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amefanya ziara ya kutembelea taasisi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambapo amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka na kujadiliana namna ya kuboresha Maonesho ya mwaka huu na miaka ijayo kuwa mazuri na yakuvutia hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa bidhaa za Tanzania.

Mhe. Prof. Mkumbo ameyazungumza hayo leo tarehe 14 Juni, 2021 alipotembelea TanTrade na kukagua matayarisho ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayotarajia kuanza tarehe 28 Juni, 2021 hadi 13 Julai, 2021 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa Lengo la Maonesho ya mwaka huu ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza biashara, bidhaa na huduma, kujifunza masuala ya biashara na teknolojia bora za uzalishaji wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa, kutengeneza mitandao ya mawasiliano itayowasaidia kukuza biashara na kupata wabia wa biashara ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Aidha Mhe. Prof. Mkumbo amekagua maeneo mbalimbali na kuridhishwa na kasi ya maandalizi ya Maonesho ya mwaka huu na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho ya mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” ikilenga kutambua mchango wa Sekta ya Viwanda katika kuchochea uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta ya kilimo katika kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na hivyo kuchangia kukua kwa uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka amezikaribisha taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kujiandaa kushiriki maonesho ya mwaka huu kwani kutakuwa na Mikutano ya Kibiashara (B2B) ambayo itafanyika kwa njia za kidigitali (Zoom Meetings) ili kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwatafutia masoko ya bidhaa na huduma mbalimbali.

Mhe. Balozi Mteule Edwin Rutageruka amesema kuwa kutakuwa na huduma ya Kliniki ya Biashara, ambayo itatolewa kwa wafanyabiashara ili kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ya ukuaji endelevu wa biashara ambayo itatolewa kwa kushirikiana na Taasisi za Umma na Binafsi zenye Mamlaka za Uthibiti na Uwezeshaji wa Biashara.

Pia TanTrade imetenga eneo maalum litakaloitwa ”Mtaa wa Kilimo” kwa lengo la kuwashirikisha wadau wa sekta ya kilimo zikiwemo Bodi za Mazao, wazalishaji wa pembejeo na teknolojia za kilimo pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kurahisisha upatikanaji wao katika eneo moja na kuwaunganisha na masoko endelevu.

Aidha, Mhe. Rutageruka amesema kuwa kutakuwepo na “Mtaa wa Madini” utakaowashirikisha wadau wote wa sekta ya madini kuanzia wachimbaji wadogo na wakubwa, watafiti na masonara kwa lengo la kupanua fursa za masoko kwa sekta hii muhimu kiuchumi.

Mhe. Balozi Rutageruka amesema kuwa usajili wa ushiriki wa maonesho ya mwaka huu unafanyika kupitia tovuti ya TanTrade ambayo ni www.tantrade.go.tz au kutembelea Ofisi za TanTrade zilizopo katika Uwanja wa Maonesho wa Mwl J.K. Nyerere Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

MWISHO.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: