Mtafiti Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima (katikati) akimuonesha Mwenyekiti wa Bodi ya TALIRI, Prof. Sebastian Chenyambuga (kulia) majani aina ya mikundekunde ambayo ni maalum kwa ajili ya kulishia mifugo yaliyopandwa katika eneo la Makao makuu ya Ofisi ya TALIRI iliyopo jijini Dodoma Juni 16, 2021. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Dkt. Daniel Komwihangilo.



 Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Profesa, Sebastian Chenyambuga (kushoto) akimueleza jambo Mtafiti Mkuu, TALIRI, Dkt. Jonas Kizima (katikati) alipokuwa akikagua mbegu ya majani ya Juncao iliyopandwa  kwenye Kitalu kilichopo katika eneo la Ofisi ya taasisi hiyo. Mwenyekiti huyo alifika katika makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dodoma jana, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasisitiza watumishi wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa bidii na kwa Weledi ili kuongeza tija katika kazi zao za kila siku.

 


Na Mbaraka Kambona,


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya tafiti za kutosha ambazo matokeo yake yaweze kutumiwa na Wafugaji moja kwa moja na sio kufanya tafiti kwa ajili ya mambo ya sayansi tu. 

Prof. Komba aliyasema hayo muda mfupi baada ya kumaliza kikao kazi cha kujadili mkataba wa utendaji kazi wa taasisi hiyo kilichofanyika katika makao makuu ya Ofisi hiyo iliyopo jijini Dodoma jana. 

Alisema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kufanya tafiti na kueneza teknolojia ya tafiti hizo ili kuendelea kuboresha tasnia ya mifugo nchini. 

"Sisi kama taasisi tumejikita katika kufanya tafiti za malisho na mbari za mifugo ili kuwafanya wafugaji waweze kufuga kwa tija na kunufaika na mifugo yao,"  alisema Prof. Komba. 

Aliongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake   atahakikisha tafiti wanazozifanya zinaendelea kuwanufaisha Wafugaji na taifa kwa ujumla. 

Aidha, Prof. Komba alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza Watendaji wa taasisi hiyo kufanyakazi kwa weledi, na kwa bidii ili waweze kuzalisha tafiti za kutosha na kuzisambaza kwa wafugaji ili waweze kuzitumia na kujiongezea kipato. 

"Tangu nimeteuliwa kuongoza taasisi hii nina miezi miwili sasa, lakini mipango yangu ni kuhakikisha  ninashirikiana kikamilifu na watafiti wenzangu ili tuweze kufanya tafiti zitakazoleta matokeo yatakayowasaidia wafugaji kupata tija na sio tafiti kwa ajili ya sayansi tu,"alifafanua Prof. Komba. 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TALIRI, Prof. Sebastian Chenyambuga alisema kuwa wajibu wa taasisi hiyo ni kufanya tafiti na hivyo aliwataka watumishi  wahakikishe wanajipanga vizuri ili kazi zao ziwe na manufaa kwa wananchi hususan wafugaji.


Share To:

Post A Comment: