Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo akisoma hotuba yake wakati wa kufunguwa semina kwa waandishi wa habari iliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuhusiana na ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kuepuka jamii kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza leo Juni 10,2021 katika ukumbi wa mikutano wa tasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe , Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Dkt. Esther Nkuba akizungumza jambo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi semina kwa waandishi wa habari kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha.kulia ni Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo.Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo, amesema kwamba waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kutoa taarifa za lishe bora pamoja na kukabiliana na magonjwa.
Dkt. Masumo amesema hayo Juni 10,2021 wakati wa kufunguwa semina kwa waandishi wa habari iliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuhusiana na ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kuepuka jamii kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yanasababishwa na ulaji usiofaa na mtindo isiyo bora ya maisha, kwa kula vyakula venye chumvi nyingi na mafuta mengi au vinywaji vyenye sukari nyingi pia ni miongoni mwa viashiria hatarishi kwa magonjwa yasiyo kuambukiza” amesema Dkt. Masumo.
Amefafanua kuwa mtindo isiyo bora ya maisha ni kutofanya mazoezi, matumizi ya sigara na tumbaku pamoja na unywaji wa pombe ambavyo usababisha mtu kupata magonjwa yasiyo kuambukiza.
Ameongeza kulingana na tafiti mbalimbali za hivi karibuni zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wenye uzito uliozidi pamoja na unene uliopitiliza.
Dkt. Masumo ambaye alikuwa anamwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, amesema kuwa pia kuna ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani pamoja na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Esther Nkuba, amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali katika mitandao ambazo sio sahihi na kujenga hofu kwa wagonjwa.
Post A Comment: