Godwin Myovela na Dotto Mwaibale,
Singida.
MKOA wa Singinda umefanya uzinduzi rasmi wa mfumo wa kielekroniki wa ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya vyombo vya moto (Parking Fees) unaojulikana kama TeRMIS.
TeRMIS yaani 'Tarura e-Revenue Management Information System' ni mfumo mpya unaolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili kusaidia matengenezo na maboresho ya miundombinu ya barabara.
Akizindua mfumo huo mkoani hapa Mkuu wa Mkoa Dkt.Binilith Mahenge amewasihi wananchi kuukubali na kuupokea mfumo huo ambao una nia njema.
Alisema lengo hasa ni kuleta ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, lakini una nia ya kumpunguzia mtumiaji wa maegesho kero ya kudaiwa ushuru.
Imeelezwa kuwa baada ya kujisajili mtumiaji ataanza kulipa mwenyewe ada za ushuru stahiki kwa siku, wiki au mwezi kulingana na mahitaji kwa kutumia mtandao wowote wa simu au tawi la Benki ya NMB, CRDB na wakala wa huduma hizo.
Dkt. Mahenge alisema unafuu mwingine wa mfumo huo ni kumsaidia mteja kufanya maombi ya kulipia huduma mahali popote alipo bila kulazimika kufika ofisi za Tarura.
Hata hivyo mkuu wa mkoa amewataka Tarura kuwa makini kwa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kina kwa waliopewa dhamana ya kukusanya mapato hayo ili kuhakikisha hakuna udanganyifu.
" Nitoe wito kwa wananchi kuyapokea mabadiliko haya na kulipa wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka tozo za faini zisizokuwa za lazima," alisema Dkt. Mahenge huku akiwataka Tarura kuhakikisha elimu juu ya matumizi ya mfumo huo mpya inawafikia wananchi ili kuwa na uelewa wa pamoja.
Akifafanua jinsi ya kufanya malipo kwa mfumo wa Termis Mtaalamu kutoka Kitengo cha Mapato Makao Makuu Tarura, Osward Mobily alisema mteja anaweza kulipia ushuru wa maegesho kwa Saa, Siku, Wiki au Mwezi.
Alieleza kwamba jinsi ya kufanya malipo mteja atalazimika kuomba mwenyewe kumbukumbu namba ya malipo kwa ajili ya kufanya malipo ya kabla kupitia namba *152*00#.
Alivitaja vyombo vya usafiri vitakavyohusika na ushuru wa maegesho hayo kuwa ni pamoja na pikipiki ya miguu mitatu kwa ushuru wa sh.300 kwa siku, Sh.1500 kwa wiki na Sh.6000 kwa mwezi.
Pia gari isiyozidi tani 2 kwa ushuru wa Sh.500 kwa siku, 2500 kwa wiki na 10,000 kwa mwezi, huku gari inayozidi tani 2 lakini isiyozidi tani 3 itatozwa Sh.200 kwa saa, Sh.1000 kwa siku, Sh.5000 kwa wiki na Sh.20,000 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Tarura gari inayozidi tani 3 itatozwa Sh.400 kwa saa, Sh.2000 kwa siku, Sh.10,000 kwa wiki na Sh.40,000 kwa mwezi, huku gharama ya Maombi ya Maegesho Maalumu yatatozwa kwa gharama ya Sh 20,000 kwa mwezi baada ya mteja kujaza fomu ya maombi au kupitia App ya TeRMI.
"Mmiliki wa chombo cha moto anatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho ndani ya siku 7 endapo atashindwa kulipa ndani ya muda atapaswa kulipa mara mbili ya kiasi anachodaiwa," alisema Mchambuzi wa Mifumo kutoka Tarura, Joseph Chigalula na akaongeza;
" Endapo atashindwa kulipa tozo hiyo pamoja na deni analodaiwa kwa muda unaozidi siku 14, atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atalipa faini ya Sh.laki tatu au kifungo miezi 12 au vyote kwa pamoja," alisema Chigalula.
Post A Comment: