Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Singida lililokutana jana kujadili majibu ya Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo  Eliya Digha  akizungumza kwenye kikao hicho.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Rashid Mandoa akizungumza kwenye kikao hicho.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Paskas Mulagiri akizungumza.

Diwani wa Kata ya Mgori Omary Mande akizungumza kwenye kikao hicho.
Madiwani wakiwa kwenye kikao hicho.

Madiwani wakiwa kwenye kikao hicho.

Madiwani wakiwa kwenye kikao hicho.
Madiwani wakiwa kwenye kikao hicho.

Mbunge wa Jimbo hilo Ramadhan Ighondo akizungumza kwenye kikao hicho
Mkaguzi wa Ndani Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Christopher Kidubo, akisoma hoja kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge, akimkabidhi Mkuu wa Polisi Wilaya ya Singida SSP John Lwamlema funguo ya pikipiki iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kama kitendea kazi katika kukabiliana na matukio ya uhalifu ndani ya Kituo Kidogo cha Polisi Kata ya Msange, Ilongero mkoani hapa.
 


Na Godwin Myovela, Ilongero


OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imepongeza kasi na maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani hapa katika kushughulikia hoja zote, isipokuwa zile za kisera, kwa kufanikiwa ndani ya muda mfupi kuzipunguza kutoka 66 hadi kufikia 27.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge, pamoja na kupongeza juhudi kubwa zinazoendelea kufanyika kwa ushirikiano kama timu baina ya watendaji, madiwani na Mbunge, aliwataka kutofanya makosa tena, badala yake waheshimu sheria za fedha na kuhakikisha hoja zilizofungwa hazijirudii tena.

Pongezi hizo zimetolewa eneo la Makao Makuu ya Halmashauri hiyo Ilongero, mkoani hapa jana, wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani lililokutana kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2020. 

"Tunawashukuru sana Wilaya ya Singida kwa juhudi hii kubwa ya kuzifunga kwa kasi ya aina yake hoja takribani 39 zilizokuwa mbele yenu. Kuhusu hoja ya upungufu mkubwa wa watumishi ambayo haijafungwa kwetu sisi tutaendelea kuiandika kama hoja mpaka itakapojifunga," alisema Mdhibiti na Mkaguzi, Nyigana Mahende.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rashid Mandoa, alisema miongoni mwa hoja zilizojitokeza na kupelekea kuitia doa huko nyuma halmashauri hiyo nyingi ni za kisera, kikanuni, uwajibikaji na ukiukwaji wa baadhi ya sheria za mawasilisho ya kifedha kitaalamu. Hakuna wizi wala ubadhirifu wowote na tayari maboresho yamekwishafanyika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Paskas Mulagiri, pamoja na kupongeza hatua hiyo aliwakumbusha watendaji wa Singida DC kwamba ili CAG afunge hoja anahitaji usahihi wa nyaraka na sio vinginevyo

"Niwasihi tuzingatie taratibu za matumizi ya fedha za serikali hasa kwenye fedha za miradi ya maendeleo bila kusababisha wala kuongeza hoja nyingine," alisema Mulagiri.

Kupitia kikao hicho Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa Katare Katare alisema alichobaini kwenye halmashauri nyingi ni kwamba hoja nyingi zinazalishwa na kushindwa kufungwa zinatokana na kasumba ya kuacha kila kitu kifanywe na watu wawili tu, ambao ni Mwekahazina na Mkaguzi wa Ndani.

"Kinachofuata hapo ni copy and paste.. ifike mahali mwenye hoja kwa maana ya aliyeibua hoja ndio abebe jukumu la kujibu hoja husika, hii itasaidia hoja kutojirudia mara kwa mara," alisema Katare.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Eliya Digha akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za kisera, alisema mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Singida ina upungufu wa watumishi zaidi ya 1000.

Digha alisema mathalani kwenye sekta ya elimu pekee kuna upungufu mkubwa wa walimu kwa asilimia 51, huku sekta ya afya ikihitaji watumishi wa haraka takribani 400...na kwenye kilimo hali ni mbaya zaidi kutokana na uwepo wa sasa wa watumishi wasiozidi 12 ambao  wanahudumia kata 21 zilizopo.

Mwenyekiti huyo maarufu Digha alisema ameguswa sana na kauli ya serikali kupitia Waziri Mkuu kuhusu ajenda ya zao la alizeti, na kwamba mkakati na shabaha iliyopo ndani ya halmashauri hiyo kwa sasa wamejipanga kuhakikisha wanapanua wigo wa kilimo hicho ili kuwa namba moja kitaifa kwa uzalishaji wake. 

"Nimuhakikishie tu Mkuu wa Mkoa wetu na Waziri Mkuu kwamba wasiwe na wasiwasi Wilaya ya Singida tumejipanga kwenye uzalishaji wa alizeti...RC na hata hiyo ruzuku ya mbegu tani 1500 uliyoomba ikija tunaomba utupendelee sisi zaidi sababu tumedhamiria kwenye alizetu, kikubwa tusaidieni tu maafisa ugani ili tuongeze tija," alisema Digha.

Katika hatua nyingine, Dk. Mahenge aliwakumbusha watendaji wote wa halmashauri na Manispaa kuweka mpango mkakati, kuainisha na kusimamia ipasavyo vyanzo vyote vya mapato sambamba na kubuni vipya, ili kuhakikisha kila chanzo kinachangia kwa asilimia 100.

Alisema kila robo ya mwaka atafanya ziara ya tathmini kupima matokeo ya agizo hilo, ikiwemo kumuwajibisha muhusika yeyote wa eneo la chanzo husika cha mapato atakayezorotesha usimamizi wake.

Kuhusu kilimo cha alizeti Dk. Mahenge pamoja na kueleza faida kubwa za kilimo hicho, alisema mpaka sasa mkoa wa Singida tayari umeomba ruzuku ya mbegu hizo takribani tani 1500 ili kufanikisha kwa tija uzalishaji wake.

"Singida tumeamua...ni lazima tuwekeze kwenye fursa ya zao la alizeti. Kuhusu changamoto za uhaba wa wataalamu wa kilimo na maeneo mengine jitihada za serikali ni kubwa na vyote hivyo vinaendelea kushughulikiwa, kikubwa tuendelee kuchapa kazi, tushirikiane na tupendane," alisisitiza Dk. Mahenge.

Share To:

Post A Comment: