Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizunguza na wajumbe  wapya wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania na watumishi wa Tume hiyo (hawapo pichani)  wakati alipofanya ziara katika tume hiyo na kuzindua bodi mpya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo juu  Ujenzi wa maabara Changamano ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Prof. Lazaro Busagala.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania  Prof. Lazaro Busagala akimuonesha Waziri Ndalichako kazi mbalimbali za nje zinazoendelea katika ujenzi wa maabara Changamano inayojengwa katika Tume hiyo jijini Arusha.
Muonekano wa hatua ya ujenzi wa Maabara Changamano iliyopo Tume ya Nguvu za Atomiki Jijini Arusha.

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetumia zaidi ya Sh Bilioni 10 kujenga maabara Changamano Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania iliyopo Jijini Arusha kwa lengo la kuimarisha upimaji wa vyanzo mbalimbali ambavyo vinakuwa na mionzi kuhakikisha vinakuwa mionzi salama.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipofanya ziara katika Tume hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo ambapo amesema maabara hiyo pia itasidia kuendeleza matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia katika maendeleo.

Waziri Ndalichako amesema maabara hiyo itakuwa na maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanyia tafiti, kuendeleza teknolojia na matumizi ya nyuklia na pia itasaidia kuangalia viasili vya mionzi kwenye vyambo mbalimbali vikiwemo vinavyotokana na huduma za tiba.

 “Maabara hii ikikamilika itakuwa kati ya maabara tano bora Afrika, na kitu ambacho ni kikubwa na muhimu katika maabara hii kutakuwa na Kitengo cha kufanya tafiti kuangalia mionzi ambayo inaweza kutumika katika tiba kwa ajili ya wagonjwa wa saratani,” amesema Profesa Ndalichako
Aliongeza kuwa maabara hii ikikamilika kama nchi itakuwa imejitosheleza katika kudhibiti na kuendeleza teknolojia ya Nyuklia na hivyo kuhamasisha uletwaji wa sampuli mbalimbali za kitafiti nchini, aidha hii itasaidia pia kutoa huduma kwa nchi jirani.

Akiwa katika Tume hiyo Waziri Ndalichako pia amezindua rasmi  Bodi mpya ya Taasisi hiyo yenye wajumbe 9 inayoongozwa na Mwenyekiti Profesa Joseph Msambichaka. Ndalichko ameagiza Bodi hiyo katika utendaji kuzingatia miongozo ya Msajili wa Hazina juu ya uendeshaji wa Bodi, huku akiwataka kuhakikisha TAEC inasogeza huduma zake kwa wananchi kwa kufungua maabara zaidi za upimaji wa viasili vya mionzi kwenye mipaka mbalilmbali nchini na kukamilisha ujenzi wa ofisi za kanda.  
Ametumia nafasi hiyo kuzitaka Bodi na  zinazosimamia Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  kuhakikisha zinasimamia mapato na matumizi ya fedha za umma kwa weledi na kuhakikisha fedha zinaelekezwa katika kutatua changamoto za wananchi na kuendeleza sekta ya Elimu.

Naye  Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TAEC Prof. Msambichaka amesema katika utekelezaji wa majukumu yao itatoa kipaumbele kusimamia ukamilishaji kwa wakati  ujenzi wa jengo la maabara Changamano ili liweze kuhudumia watanzania na nchi za jirani kwa viwango vya kimataifa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume za Nguvu za Atomiki nchini Prof. Lazaro Busagala amesema ujenzi wa maabara changamano umefadhiliwa na serikali kwa asilimia mia moja na kwamba  jengo hilo litakuwa na maabara nane, maabara za kupima  viasili vya mionzi, maabara za uchunguzi na utafiti wa viasili vya mionzi kwa ajili ya matibabu ya saratani,  maabara ya utengenezaji vifaa vinavyotumia vifaa vya mionzi au vifaa vya nyuklia, maabara ya upimaji wa viwango vya mionzi kwenye simu na minara ya simu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: