Wizara ya Maliasili na Utalii imemteua Rawan Dakik kuwa balozi wa hiari wa Mlima Kilimanjaro ikiwa ni kutambua jitihada zake za kutangaza Mlima Kilimanjaro nchini baada ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa takriban mara tano na pia kuipeperusha bendera ya Tanzania katika kilele cha mlima mrefu zaidi duniani Everest uliopo bara la Asia.
Naibu Waziiri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo wakati wa hafla fupi ya mapokezi ya Rawan Dakik iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro leo.
“Ni jambo la kujivunia sana leo hii kwa bendera yetu ya Tanzania kupeperushwa na si tu mwanamke wa kwanza kabisa Mtanzania lakini pia Mwanamke mwenye umri mdogo zaidi kufika kilele cha mlima Everest kutoka bara la Afrika”ameongeza Mhe. Masanja.
Mhe. Mary Masanja amesema kuwa Rawan Dakik amefanikiwa kufika katika kilele cha mlima Everest kutokana na jitihada binafsi alizojijengea baada ya kuanza kupanda Mlima Kilimanjaro tangu akiwa na umri wa miaka 13 kwa takriban mara tano.
”Mlima wetu wa Kilimanjaro umekuwa chachu ya mafanikio ya Rawan Dakik kwa kufika kilele cha mlima Everest kwa kuwa wataalam wanasema mlima Kilimanjaro ni moja ya kipimo muhimu cha kumuwezesha mtu kufanikiwa kupanda mlima Everest.” amesema Mhe. Mary Masanja.
Aidha, amesema mafanikio ya Rawan Dakik yatatoa hamasa kwa vijana wa Kitanzania hususan wasichana kutimiza ndoto zao.
Post A Comment: