Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipokuwa akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Km 3.2), mkoani Mwanza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Eng. Patrick Mfugale ambaye alikuwa akielezea hatua za ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa Kilometa 3.2 linalounganisha kati ya Wilaya ya Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza ambapo limefikia asilimia 27, huku Daraja la kupitisha vifaa likiwa limekamilika kujengwa kwa asilimia 100.

Nondo zilizosukwa kwa umbo la duara zikishushwa ndani ya moja ya shimo refu lililochimbwa ndani ya maji ya ziwa Victoria katika hatua zinazoendelea za ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa Kilometa 3.2 Kigongo mkoani Mwanza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia ujenzi wa moja na Nguzo ambayo imeshawekewa zege katika muendelezo wa kazi za ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa Kilometa 3.2 Kigongo mkoani Mwanza.

Taaswira ya ujenzi wa Nguzo katika Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa Kilometa 3.2 Kigongo mkoani Mwanza.

Ujenzi wa Daraja la kupitisha vifaa vya ujenzi ukiwa umekamilika kwa 100% huku ujenzi wa Daraja la JP Magufuli ukiendelea kwa kasi kubwa ambapo sasa umefikia asilimia 27.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM linalojengwa katika eneo la Kigongo hadi Busisi jijini Mwanza.

Akizungumza na wananchi upande wa Sengerema mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja hilo, Rais Samia alisema kuwa nia ya Serikali ni kulifanya jiji la Mwanza kuwa Kitovu cha Biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.

“Daraja la JPM litarahisisha huduma za usafiri na pia kupunguza muda wa kuvuka katika Ziwa hilo tofauti na ilivyo sasa ambapo wasafiri wanatumia muda mrefu kusubiri kivuko na ili kupata huduma ya kuvuka”, alisema Rais Samia.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alimuahidi Rais Samia kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia ujenzi wa Daraja la JP Magufuli kwa karibu ili kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba ili wananchi waweze kunufaika na mradi huo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mheshimiwa Rais naomba nitumie fursa hii kukukaribisha katika eneo la mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli. Wizara inashirikiana vizuri na wenyeji wa eneo hili katika kuendeleza mradi huu ambapo hadi sasa ajira kwa ajili ya usaidizi wa ujenzi wa daraja hili zimetolewa kwa wakazi wa hapa Sengerema, Misungwi pamoja na maeneo mengine ya jiji la Mwanza, hivyo wakazi wa eneo hili tayari wameanza kuonja matunda ya mradi huu”, alisema Dkt. Chamuriho.

Awali akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, alimueleza Rais Samia kuwa Daraja la JPM lenye urefu wa Kilometa 3.2 na upana meta 28.45 ambalo pia linahusisha ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa Kilometa 1.66 linagharimu shilingi Bilioni 716 na kwamba hadi sasa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 27.

“Mhe. Rais kama utakavyojionea daraja la muda tayari limekamilika kwa asilimia 100 na sasa magari yanaweza kuvuka kwenda Busisi na kurudi, daraja hili la muda limejengwa kwa ajili ya kurahisisha shughuli za ujenzi wa daraja kubwa”, ameeleza Mhandisi Mfugale.

Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo kukamilika kwake kutarahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani mikoa ya Mwanza, Geita pamoja na nchi jirani.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: