SAKATA la wizi wa sh. bilioni 1.6 ulioibuliwa Mei 28 mwaka huu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Wizara ya Fedha na Mipango limetua bungeni baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kutaja kiini cha wizi huo huku akimpongeza Majaliwa kwa kuibua sakata hilo.
Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni Dodoma, Mpina amesema wizi wa aina hiyo umekuwa ukiandaliwa kwa muda mrefu kuanzia hatua ya awali ya upangaji wa bajeti na kushauri Serikali kumulika eneo hilo.
Mpina amesema ni jambo la kusikitisha kuona wizi wa aina hiyo unatokea na kunufaisha watu wachache huku wananchi wengi wakikabiliwa na changamoto nyingi kwenye sekta za afya, maji, barabara, elimu lakini fedha zinatafunwa na kikundi kidogo cha watu.
“Mheshimiwa Spika jambo jingine ni tathmini ya matumizi ya OC hivi tunapo bajeti kila mwaka matumizi ya OC siku zote yamekuwa kwa mwendo wa ukomo wa bajeti, mwendo wa ukomo wa bajeti wanazungumzia tu ukomo wa bajeti kwamba mwaka huu bajeti imeongezeka kwa asilimia 5 imepungua kwa asilimia ngapi lakini huu mwenendo tutaenda nao mpaka lini kwanini OC zisitolewe kwa umuhimu wa mahitaji ya kila wizara” amesema Mpina
Mpina amesema kitendo cha kutopanga fedha kutokana na umuhimu wa mahitaji ya wizara kumesababisha kuwepo kwa mianya ya matumizi yasiyo ya lazima na kutokea wizi na ufujaji mkubwa wa fedha za Serikali.
“Matokeo yake katika hili eneo tumekuwa kukipoteza fedha nyingi sana na wizi mwingi unaadaliwa kwenye bajeti pesa zinaandaliwa zinawekwa fungu mahususi kwa ajili ya kuchotwa baadae na mfano wake ndio hili dubwasha la Sakata ambalo ameliibua Waziri Mkuu katika Wizara ya Fedha bilioni 1.6 zimepigwa pale na huu ni mkakati ambao umeandaliwa kuanzia kwenye bajeti”alisema Mpina
Kufuatia hatua hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa kuibua mtandao huo wa wizi ndani ya Wizara ya Fedha, Mpina amempongeza kwa kubaini wizi huo na hicho ni kielelezo cha wizi unaondelea maeneo mbalimbali nchini.
“Hapa na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kasim Majaliwa Majaliwa kwa kuliibua hili sakata lakini Mh Spika sakata hili mwanzo wake ni mipango ambayo imeandaliwa kutoka kwenye bajeti fedha zimeludhikwa kwenye kazi fulani kazi ambayo haina umuhimu na mwisho wa siku ni lazima zile fedha zitumike kugawanwa kwa sababu njama zimefanyika kuanzia kwenye mpango wa bajeti”alisema Mpina
Hivyo Mpina akahoji bungeni kuwa kwa taifa kama hili tutaendelea kuwa na mipango ya namna hiyo mpaka lini na kwanini hizo oc zisipangwe kwa umuhimu wa matumizi kwa wizara na sio kutumia mfumo wa ukomo wa bajeti ambao umekuwa ukitengeneza wizi wa aina hiyo.
“Wizara inahitaji tumizi hilo kwa ajili ya jambo gani tukajiridhisha nacho kuliko ilivyo hivi sasa kwamba tunazungumza tu ukomo wa bajeti , ukomo wa bajeti basi fedha zinaidhinishwa Mh Spika tukienda kwa namna hiyo kwa taifa changa lenye mapato madogo kama haya tutapata matatizo makubwa sana”alisema Mpina
Hata hivyo sakata hilo liliungwa mkono na wabunge wengine hali iliyomfanya Spika Bunge, Job Ndugai kuingilia kati na kuwaomba wabunge wawe wavumilivu wakati suala hilo likiendelea kuchunguzwa.
“Waheshimiwa wabunge kuhusu hili suala la wizara ya fedha na matumizi yaliyofanyika kama Mh Waziri Mkuu alivyowatembelea ningeomba kwa sasa tusiwahukumu kwa sababu bado ni jambo linalofanyiwa kazi alafu taarifa itapelekwa kwa Mh Waziri Mkuu labda baadae tutakuja kupata taarifa halisi sasa kwa kuwa linafanyiwa kazi tukipitisha hukumu kabisa nadhani tutakuwa a little bit unfair kwa hiyo ningewaomba tuliache kidogo”alisema Ndugai.
Post A Comment: