WAZIRI Mkuu Mstaafu, John Malecela, amemshauri Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Antony Mtaka, kutilia mkazo sekta ya ufugaji kwa kuwa mkoa huo una idadi kubwa ya mifugo.
Juzi Mtaka alimtembelea Mzee Malecela nyumbani kwake eneo la Uzunguni jijini Dodoma na katika mazungumzo yao, Malecela alisema idadi kubwa ya mifugo mkoani Dodoma ni fursa muhimu katika kukuza uchumi.
Alisema fursa ya mifugo mkoani Dodoma unakwenda sambamba na kilimo cha alizeti na karanga Ili kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini.
Alisema ingawa mkoa una Kituo cha Utafiti wa Mifugo cha Mpwapwa na Shamba la Mifugo (Ranchi) la Serikali la Kongwa, rasilimali hizo hazijatumika ipasavyo kusaidia kuzibadili jamii za wafugaji wa mkoani humo kupata tija kwani bado wanafuga kienyeji.
Kwa mujibu wa Malecela, Mkoa wa Dodoma una fursa kubwa ya kilimo cha mazao yanayokamuliwa na kuzalisha mafuta ya kupikia hususan katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa huku wilaya nyingine zikisifika kwa kilimo cha alizeti na zabibu.
Katika mazungumzo yao, Mtaka, alimshirikisha Malecela vipaumbele vyake mkoani hapa na kumshukuru kwa ushauri aliompa.
Alisema kipaumbele cha kwanza ni elimu na kwamba, kazi iliyo mbele ni kunyanyua kiwango cha elimu na ufaulu katika mkoani Dodoma.
Kipaumbele kingine kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo ni kilimo kwa kuzifanya wilaya za pembezoni kuwa kanda maalum za kilimo ili kilimo mkoani Dodoma kiwe cha kibiashara.
Alisema ili kufanikisha azma hiyo, atatia mkazo zaidi katika kilimo cha zabibu, alizeti na mazao mengine yanayozalisha mafuta ya kupikia.
Alisema kumekuwa na mahitaji makubwa ya mafuta ya kupikia yanayoilazimu nchi kuagiza mafuta nje ya nchi.
"Hii ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa mkoa wetu unaozalisha mazao yanayotumika kuzalisha mafuta kama alizeti, karanga na ufuta," alisema.
Katika hatua nyingine; Mtaka alisema ataendesha kampeni ya mkoa ya upandaji na ustawishaji miti itakayoshirikisha wadau mbalimbali tangu ngazi ya kaya hadi mkoa
Alimtaja Malecela kama mfano wa kuigwa wa wanamazingira waliofanikisha kupanda miti mingi katika maeneo waliyoongoza.
Post A Comment: