Ofisa Lishe Mkoa wa Singida,  Teda Sinde akifafanua jambo kuhusiana na suala zima la Lishe.
Mama anayezingatia suala la Lishe bora akimlisha mwanae huku mtoto akifurahia chakula anacholishwa.
Baadhi ya watoto wenye udumavu.



Na Abby Nkungu, Singida


TATIZO la lishe duni bado ni changamoto kubwa mkoani Singida kutokana na takwimu kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 29 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 wanaendelea kukabiliwa na udumavu.

Katika kipindi hiki ambapo dunia  inaadhimisha “Siku ya Kimataifa ya Chakula Salama”, taarifa  ya Ofisa Lishe mkoa wa Singida,  Teda Sinde inaonesha kuwa mbali na udumavu, asilimia 5.2 ya watoto  wote wenye umri huo wana ukondefu na asilimia 18 wakiwa na uzito pungufu.

"Tatizo hilo linasababishwa na ulaji duni usiozingatia makundi matano ya chakula pamoja na idadi ya milo inayotakiwa kwa siku na magonjwa kama Kifua Kikuu, Ukimwi na Kuharisha" anafafanua Teda na kuongeza;

Watoto kutokunyonyeshwa kwa kuzingatia kanuni za unyonyeshaji ambazo ni unyonyeshaji wa miezi sita ya mwanzo bila kumpa mtoto chakula chochote; hata maji, isipokuwa dawa kwa maelekezo ya mtaalamu wa afya, ni sababu nyingine za udumavu, uzito pungufu na ukondefu".

Alieleza kuwa hali hiyo huathiri ukuaji wa ubongo; hivyo kusababisha mtoto kutokufundishika kirahisi darasani na kuwa mzito kwenye kufikiria na hata  kutoa uamuzi pindi anapokuwa mtu mzima.

Teda alisema kuwa  matatizo hayo  pia  husababisha upungufu wa damu mwilini, huathiri mfumo wa kinga  mwilini katika kupambana na magonjwa, huchangia mtoto kupata utapiamlo na magonjwa mengine pia huweza kusababisha kifo.

Baadhi ya wazazi na walezi waliohojiwa na Mwandishi wa habari hizi, akiwemo Miriam Makita na Sikudhani Hamisi wanasema tatizo la udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Singida linachangiwa na elimu duni miongoni mwa jamii juu ya suala zima la lishe bora.

Aidha, walisema kuwa imani potofu juu ya ulaji wa wajawazito na watoto kwa baadhi ya vyakula ikiwa ni pamoja na maini, mayai na vyakula vingine vyenye virutubisho muhimu mwilini, huchangia katika kuleta madhara hayo.

Walitoa  mwito kwa wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu zaidi juu ya lishe  bora; hasa maeneo ya vijijini ambako kuna vyakula vingi vya asili vyenye virutubishi muhimu vinavyoweza  kufaa kuboresha afya kwa mama mjamzito na mtoto; hivyo kutokomeza utapiamlo.

Naye, Kaimu Ofisa elimu Manispaa ya Singida, Albert Clement alisema asilimia 90 ya shule za msingi katika halmashauri hiyo hawatoi huduma ya chakula mchana kwa wanafunzi wao kutokana na wazazi wengi kuwa wagumu kuchangia kwa kile kinachodhaniwa kuitafsiri isivyo sahihi dhana ya 'Elimu bure'.

"Japo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huondoka shuleni mapema kurejea nyumbani, siwezi kusema kwa yakini iwapo watoto hao hupata chakula wanachostahili wafikapo majumbani mwao" alisema Kaimu Ofisa elimu huyo. 

Share To:

Post A Comment: