Na Jackline Kuwanda, Dodoma.


Imeelezwa kuwa Tanzania siyo nchi ya kwanza kuacha lugha ya kigeni na kutumia lugha yake ya kiswahili katika utoaji wa haki.


Akifungua Mkutano wa wadau leo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda amawataka washiriki kujadili mchango wa Kiswahili katika upatikanaji na utoaji haki nchini.


Amesema kuna nchi nyingine ambazo zimekuwa zikitumia lugha zao rasmi katika kutoa haki ikiwemo India na zimekuwa zikifanya vizuri katika eneo hilo


“Ziko nchi wanatumia lugha zao katika uandishi wa sheria na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za haki, ifahamike kuwa asili ya lugha ya kisheria si kiingereza kama inavyofahamika na wengi bali lugha za kijerumani, kilatini na kifaransa kwa kuwa waliionekana kustaarabika’’amesema Pinda


Aidha, Pinda amesema licha ya lugha ya Kiswahili kuwa moja ya nguzo inayosimamia ukuaji wa uchumi,  serikali iliona umuhimu wa kuanza kutumia lugha hiyo katika utoaji na upatikanaji wa haki nchini ambapo sheria nyingi ziko kwa kiingereza ambayo imeonekana kuwa ni changamoto katika upatikanaji wa haki.


Naibu Waziri amewataka wanasheria kujikita na kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji wa haki.


‘’Niwaombe wanasheria kutumia lugha ya Kiswahili kuna watu wamekosa haki zao sababu hawafahamu lugha , ni wakati sasa kwa watanzania kutumia lugha yetu, hatuwezi kutumia lugha ambazo si zakwetu’’


Pinda amesema Kiswahili ni lugha ya kimataifa ikiwa ya kumi duniani yenye wazungumzaji wengi Barani Afrika na duniani kote.


Ameongeza kuwa Wizara inaratibu ukuzwaji na uendelezaji wa matumizi ya lugha ya ksiwahili katika utoaji haki, kuratibu wasimamiaji haki katika sekta nyingine katika kutekeleza na kutoa haki nchini.


‘’Wizara ya katiba na sheria inaratibu zoezi la kutafsiri sheria zote kwa lugha ya Kiswahili,mchakato wa kutafsiri unafanywa ndani ya Wizara pamoja na taasisi zake’’amesema Pinda


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju amesema lengo la mkutano huo ni kujadili matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mfumo wa utoaji haki.


‘’tumeona tukutane na wadau wenye ubobezi wa lugha hii ya Kiswahili ili tuje na misamiati itakayokubalika katika mfumo wa utoaji haki lakini pia tunahakikisha tunapata lugha sahihi ya Kiswahili tutakayoitumia katika mfumo wetu wa utoaji haki’’amesema Mpanju


Akishukuru kwa niaba ya washiriki, Mwalimu  Asina Omari kutoka Shule kuu ya Sheria chuo kikuu cha Dar es salaam amesema watahakikisha kuwa wanakuwa na sheria ambazo zitasaidia wananchi kupata haki zao.


‘’maekezo ambayo tumepatiwa tutakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kupitia sheria’’amesema Asina.


Mnamo tarehe 24/1/2021 Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihudhuria ufunguzi wa Maadhimisho ya wiki ya sheria,aliasa kuwa ni vyema sheria za uendeshaji wa kesi mahakamani ukawa kwa lugha ya kiswahili.


Ikumbukwe kuwa Hayati Dkt John Pombe Magufuli wakati wa uhai wake alijipambanua katika matumizi ya lugha ya Kiswahili ambapo hotuba zake nyingi alizitoa kwa Kiswahili ambapo alihimiza umuhimu wa Kiswahili katika mfumo wa sheria na utoaji haki nchini katika nyakati tofauti.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: