Nteghenjwa Hosseah, Chemba


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amemaliza mgogoro wa kiutalawa uliodumu kwa muda mrefu na kufanya kuzorota kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Chemba.


Waziri Ummy amemaliza mgogoro huo kwa kuondoa tofauti za waheshimiwa madiwani na wataalamu wa Chemba na kuwataka kuwa kitu kimoja, kufanya kazi kwa kushirikiana, kuheshimiana na kupendana.


Waziri Ummy aliingilia kati  mgogoro huu baada ya ziara yake aliyoifanya tarehe 04/05/2021  kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na kamati ya Fedha pamoja na Menejimenti ya Wilaya ya Chemba na kubaini viashiria vya mgogoro katika halmashauri hiyo.


Katika kikao alichokifanya mapema leo hii Waziri Ummy aligundua  chanzo cha mgogoro huo ni mgawanyiko mkubwa baina ya waheshimiwa madiwani na Timu ya Menejiment ya Halmashauri hiyo sambamba na Menejimenti hiyo kutokuwa pamoja.


Pia ushirikishwaji mdogo wa  madiwani katika baadhi ya maamuzi ya Halmashauri na kutokulipwa stahiki zao kwa kipindi kirefu kitu ambacho kimechochea kuzalisha madeni yanayoathiri utendaji kazi.


Aidha, ukusanyaji usioridhisha wa makusanyo ya ndani na matumizi yasiyo sahihi ya mashine za kukusanyia mapato (POS) pamoja na kuchelewa kupeleka makusanyo Benki na matumizi ya fedha mbichi.


Halkadhalika aligundua upelekaji mdogo wa fedha kwenye miradi ya maendeleo na kuwa fedha hizo za maendeleo hazitumiki katika shughuli za maendeleo ila hutumika kwa ajili ya posho za safari, vikao na semina.


Baada ya majadiliano ya muda mrefu Mhe. Waziri alitoa maagizo kwa halmashauri zote nchini,  kuwa Madiwani na Wataalam kila mmoja kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha wanaheshimiana na kuthamiana wakati wote.


Pia amezitaka kila Halmashauri kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri na kuhakikisha kuwa asilimia 40 ya fedha zinazokusanywa zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ambayo inagusa wananchi moja kwa moja kama shule, hospitali, masoko nk.


“Nawakumbushe Halmashauri zote nchini  kuwa fedha za maendeleo nataka ziende kwenye maendeleo, miradi ile ambayo inatatua changamoto za wananchi moja kwa moja kama madarasa, madawati, matundu ya vyoo, zahanati, vituo vya afya na sio kulipana posho za safari, vikao au semina” alisema Ummy.


Pia aliwataka watendaji wote waliopewa dhamana ya kukusanya mapato ya ndani ya halmashauri kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia weledi, uaminifu na uadilifu katika kutekeleza jukumu hilo na yule atakayekwenda kinyume na hapo atamtoa haraka sana katika nafasi hiyo.


Aidha Waziri Ummy pia alisisitiza kuongeza udhibiti wa mifumo ya kukusanyia mapato katika halmashauri (Internal Control) na kuhakikisha watumishi wote wanaokabidhiwa mashine zote za kukusanyia mapato (POS) wasitoe username wala password kwa mtu mwingine yeyote hata kama ni bosi.


Pia Waziri Ummy aliwataka watumishi wote wanaokusanya mapato kuhakikisha wanapeleka fedha za makusanyo benki ndani ya masaa 24 baada ya kufanya usuluhisho na kutoa ankra ya malipo kutoka kwa mhasibu wa halmashauri.


Pia Waziri Ummy aliahidi kwenda kufanyia kazi changamoto ya madeni ya  madiwani ya kutokulipwa posho zao za mwezi kwa wakati.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: