Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza na Wazee wa Manispaa ya Singida kwa mara ya kwanza tangu ahamishiwe akitokea mkoani Dodoma katika kikao kilicho fanyika leo. Kulia ni .Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wilaya ya Singida, Ramadhan Maughu na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi,akizungumza kwenye kikao hicho.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.
BARAZA la Wazee Mkoa wa Singida limempokea rasmi Mkuu mpya wa Mkoa, Dkt. Binilith Mahenge na kuahidi kumpa kila aina ya ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
Dkt. Mahenge ambaye kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliteuliwa na kuapishwa hivi karibuni kushika wadhifa huo kuchukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amestaafu.
Akizungumza na baraza hilo mkoani hapa, Dkt. Mahenge aliwaomba wazee hao kumpa ushirikiano ili kwa pamoja aweze kuongoza kwa ufanisi jahazi hilo lenye shabaha ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani ya mkoa.
"Singida ina kila kitu chema. Tuna Hali ya hewa nzuri inayokubali kila aina ya mazao...alizeti, ufuta, dengu, korosho na tunafuga sana, lakini zaidi tuna viwanda vya kutosha vya kukamua mafuta ya zao la alizeti," alisema Mkuu wa Mkoa.
Alihimiza kila mtu kwa nafasi yake likiwemo kundi la vijana, watendaji na wananchi wote kuwajibika kwa kuchapa kazi ili kupunguza au kuondoa kabisa adha ya umasikini.
Dkt. Mahenge pamoja na kumshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumkabidhi mkoa huo kikubwa alisisitiza ushirikiano hususani kwenye nyanja ya kuinua sekta ya kilimo-na hasa zao la alizeti.
Alisema anatarajia kuona mtazamo chanya katika mageuzi makubwa ya kilimo cha alizeti katika muktadha wa kuleta utajiri kwa kila mtu, kaya, jamii, lakini pia kuigeuza Singida kuwa kimbilio la soko kama sehemu ya jitihada zilizopo katika kukabiliana na changamoto ya kitaifa ya uhaba wa mafuta ya kula.
Akieleza hali halisi ya zao hilo mkoani hapa kwa sasa, alisema changamoto kubwa inayokwamisha ustawi wake kwanza ni uhaba wa mbegu bora, lakini pia wakulima wengi wamekosa utaalamu stahiki kujua kanuni za kilimo chake.
Mahenge alisema kwa ushirikiano na watendaji wake waliopo watahakikisha wanaongeza nguvu katika eneo hilo na lingine la kutoa utambuzi kwa mkulima kumuwezesha kufanya Uchaguzi sahihi wa mbegu zinazotoa kiwango cha juu cha mafuta na zinazohimili magonjwa yatokanayo na visumbufu vya wadudu.
Katika hilo, mkakati mwingine uliopo ndani ya ofisi yake kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali za kilimo ni kuhakikisha mbegu hizo zinaanza kupatikana kwa wingi na kuwafikia wakulima kwa gharama nafuu.
"Tatizo lililopo ukilinganisha na mazao mengine alizeti haina Bodi ya uratibu na usimamizi ndio mana hata kasi ya ukuaji wake haiendi kwa ufanisi," alisema Dkt. Mahenge na akaongeza;
"Wakulima wengi wanapopeleka zao hili sokoni wanaonekana kama wamepunjwa sababu kubwa ni mbegu kukosa sifa na ubora wa kutoa mafuta mengi."
Alisema, mathalani, mbegu bora ya alizeti ijulikanayo kama Hysun 33 ambayo hukomaa kati ya siku 90 na 110 kwa uwezo wa kutoa gunia 16 hadi 22 kwa heka, sawa na uwiano wa lita 29 hadi 31 bei yake bado ipo juu na wakulima wengi wanashindwa kumudu.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo uliobeba hotuba hiyo iliyoashiria mikakati, matarajio na mwelekeo wa vipaumbele kadhaa kwa niaba ya wazee, Mwenyekiti wa Baraza hilo Ramadhan Maughu alimhakikishia Mkuu wa Mkoa ushirikiano wa hali ya juu katika azma iliyopo ya kubadilii sura ya kiuchumi ya mkoa.
""Karibu sana Singida wazee wote mbele yako wamekukubali na wamekupokea tutakupa kila aina ya ushirikiano, mana hatukuzoea wala kuwahi kuitwa na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa yeyote..kwa utambuzi huu inaonyesha umelelewa vizuri," alisema Mwenyekiti huyo.
Post A Comment: