Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fredy Lowassa (kushoto) walipokutana katika kikao kilichoandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kilichofanyika jijini Dodoma jana. Mbunge huyo alikuwa ni miongoni  mwa Wawekezaji waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Sehemu ya Wawekezaji waliohudhuria kikao kilichoandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) jijini Dodoma jana. 
 



Na Mbaraka Kambona,

 

Wawekezaji wa muda mrefu katika Vitalu vya Ranchi za Taifa wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti uvamizi unaofanywa na baadhi ya Wananchi katika maeneo hayo kwani vitendo hivyo vimekuwa kikwazo kikubwa katika kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini. 

Wawekezaji walisema  hayo kwa Waziri wa Mifugo na  Uvuvi, Mashimba  Ndaki alipokutana nao katika kikao kilichoandaliwa na Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO)  kilichofanyika jijini Dodoma jana. 

Wakieleza changamoto wanazozipata katika uwekezaji wao walisema kuwa pamoja na mambo mengine, suala la Wananchi kuvamia maeneo yao waliyowekeza linakwamisha kufanya shughuli zao za kuendeleza ufugaji wa kisasa. 

Mwenyekiti wa Wawekezaji hao, Jackson Mwasonga alisema kuwa wavamizi wanakwamisha shughuli zao na kuna wakati wanalazimika kutoa hela kwa wavamizi hao ili waweze kuchunga mifugo yao katika maeneo wanayomiliki kihalali. 

"Mhe. Waziri inafika wakati tunatoa hela ili tuweze kuchunga na kunusuru mifugo yetu,uvamizi unatishia maisha yetu na mali zetu, tunaomba mtangaze wavamizi waondoke ili tuweze kufanya ufugaji unaohitajika kwa amani," alisema Mwasonga. 

Projestus Gamasho, Mwekezaji katika Ranchi ya Kitengule, Mkoani Kagera alisema ranchi hiyo kwa sasa imevamiwa na tembo zaidi ya Mia Sita (600) na wameharibu miundombinu yote huku akiiomba Serikali kutoa msaada wa haraka kuwaondoa tembo hao. 

Mwekezaj wa Ranchi ya Uvinza, Kigoma, Benard Katamba  alisema wavamizi katika Ranchi hiyo sio tu wamechukua maeneo yao,  wanaiba mifugo yao kila wakati jambo ambalo linawakatisha tamaa ya kuendelea na ufugaji. 

Sisi Wawekezaji wa Ranchi ya Uvinza tumevamiwa haswa, mpaka sasa nimeshaibiwa ng'ombe 25 na mbuzi 150 na sina matumaini yoyote ya kuwapata, kwa kweli tunaomba msaada wa Serikali," alisema Katamba. 

Kufuatia hali hiyo, Mwekezaji katika Ranchi ya Misenyi, Mkoani Kagera, Nestory Lugakingira akitoa ushauri kwa Serikali alisema kuwa ili waweze kuishi kwa amani Serikali ione uwezekano katika yale maeneo yaliyovamiwa yagawiwe kwa wavamizi hao na sehemu itakayobaki waitumie kuendeleza mifugo yao na kuepuka migogoro na wananchi hao. 

Akitoa ufafanuzi wa hoja za Wawekezaji hao, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema kuwa Serikali ipo pamoja na Wawekezaji hao na itachukua hatua kali kwa wale wote wanaovamia maeneo ya ranchi kinyume na Sheria. 

"Ninaelewa kwamba kuna maeneo ambayo Wananchi wanakaa na kuwaondoa itakuwa ni uvunjifu wa haki za binadamu, maeneo hayo tutayainisha na ili tuone kama tunataka kuendelea nayo au tukubali  maeneo hayo yawe na matumizi mengine," alisema Ndaki. 

Aidha, Ndaki alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wawekezaji hao kuyatumia maeneo waliyowekeza kwa malengo yaliyokusudiwa huku akisema kuna baadhi ya Wawekezaji wamekuwa hawayatumii vizuri maeneo hayo jambo lililopelekea kuvamiwa. 

"Niwaombe kuanzia sasa mkayatumie maeneo hayo kwa malengo yaliyokusudiwa, mkafanye ufugaji wa kibiashara, mkifanya hivyo mtaweza kuainisha vizuri gharama za matumizi na faida mnayopata," alisisitiza Ndaki. 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO, Paul Kimiti  alisema uvamizi unaoendelea unawaumiza Wawekezaji  na kuwakatisha tamaa huku akiiomba Serikali kuchukua hatua kudhibiti vitendo hivyo. 

Naiomba Serikali kuangalia uwezekano wa NARCO kuwa na Askari kama TANAPA, naamini watasaidia kudhibiti uvamizi huu kabla haujashamiri, na vitendo hivyo vitakoma," alisema Kimiti 

Lengo la kikao hicho kilichoandaliwa na NARCO ni kuongea na Wawekezaji hao kuhusu Tozo mpya ya pango ya kitalu itakayoanza kufanyakazi Julai 1, 2021 na kuwahimiza kuhuisha mikataba yao.


Share To:

Post A Comment: