Mwandishi wetu,Simanjiro
Wananchi wa kijiji cha Landanai wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamepinga vikali hukumu ya kesi iliyompatia ushindi mkazi mmoja wilayani humo, Klembu Laizer huku wakiziomba mamlaka za juu kuingilia kati.
Wananchi hao wamepinga hukumu ya kesi hiyo ya ardhi nambari 10 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa na Laizer dhidi ya mwakilishi wao Ololubare Nginyu ambayo iliamuliwa hivi karibuni na Jaji wa mahakama kuu kanda ya Arusha kitengo cha ardhi, Jaji MASARA.
Katika kesi hiyo Laizer alifungua mashtaka dhidi ya Nginyu kwa madai amevamia shamba lake lenye ukubwa wa ekari 1000 na kusababisha athari mbalimbali huku akitaka alipwe fidia ya kiasi cha zaidi ya sh, 500 milioni.
Nginyu pamoja na wakazi wa kijiji cha Landanai wameshangazwa na hukumu hiyo kwa kuwa yeye anakiri kuishi kwenye eneo la ekari 50 tu ambazo alipewa kihalali na serikali ya Kijiji cha Lendanai.
“Pamoja na ushahidi tulioutoa mahakamani lakini Jaji hakuuzingatia na kuamua kutoa ardhi ya Kijiji chetu kwa mfanyabiashara huyo kwa kuhalalisha mipaka isiyotambulika hata na GN za Serikali”alisema Nginyu
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Landanai wamepinga vikali hukumu hiyo wakidai ya kwamba shamba alilopewa Laizer ni mali halali ya kijiji cha Landanai na kwamba Bw. Laizer ametapeliwa kwa kuuziwa kibatili na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji kingine.
Moses Kemuli alisema kwamba hukumu iliyotolewa na mahakama haikutenda haki kwa kuwa hatua za ugawaji wa shamba husika ulikuwa ni batili kwa kuwa waliogawa shamba hilo hawakuwa viongozi wa kijiji cha Landanai.
“Laizer alinunua hilo shamba ambalo ugawaji wake ulikuwa batili kwasababu waliogawa hawakuwa viongozi wa kijiji cha Landanai na hawakuwa na mamlaka kisheria kugawa ardhi ya kijiji kingine” alisema mkazi huyo.
Mkazi mwingine,Joseph Lairumbe alienda mbali zaidi na kupinga hukumu hiyo kwa kudai kwamba Machi 6 mwaka jana serikali ya mkoa chini ya Uongozi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Alexander Mnyeti iliamwamuru Laizer akabidhi shamba hilo kwa serikali ya kijiji cha Landanai ndani ya siku 14 kwa kuwa sio mali yake kulingana na mipaka halali iliyogawa Vijiji .
Mkazi huyo alidai kuwa matumizi ya shamba hilo yaliamriwa yatolewe na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro maagizo yaliyotekelezwa kugawa Ardhi hiyo kwa wakati kwa Kijiji cha Lendanai kutokana na maombi na mahitaji ya wakazi hao.
Baadhi ya viongozi wa kijiji cha Landanai walipinga hukumu hiyo vikali huku wakidai kwamba kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Naberera na Longai kuuza ardhi yao hovyo na sasa wamehamia kijijini kwetu na kuwauzia watu kinyemela jambo ambalo limeibua migogoro mingi ya ardhi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Landanai, Joshwa Oimbia alisema kwamba yeye kama kiongozi wa kijiji anapinga vikali hukumu hiyo kwa kuwa eneo alilopewa Laizer ni mali halali ya serikali ya kijiji changu huku akisisitiza kwamba ametumia kazi kubwa kuwazuia wananchi wenye hasira kutolivamia mpaka sasa.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa kijiji cha Naberera kuuza hovyo ardhi kwa wafanyabiashara wa madini sasa wamemaliza ardhi ya kijiji hao sasa wamevamia kwetu wanawauzia watu kinyemelea na kusababisha migogoro ya mara kwa mara serikali lazima iingilie kati kwasababu hukumu hii inahalisha unyang’anyi huo na uvunjifu wa sheria y ardhi za vijiji”, alisema kiongozi huyo.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Alaika, Mathayo Milya alisema kwamba serikali isipokuwa makini hukumu hiyo huenda ikasababisha maafa makubwa kwa kuwa vyombo vya uchunguzi vilipaswa kujiridhisha kwa kukagua mipaka ya ardhi halali eneo husika linalogombaniwa kabla ya kutoa hukumu husika.
Hatahivyo, alisisitiza kuwa wananchi pamoja na viongozi husika wamepanga kukata rufaa ya hukumu hiyo kupinga maamuzi yote huku wakijipanga kumwandikia barua Jaji Mkuu nchini ili kumuelezea changamoto na dosari zote zilizojitokeza katika kesi hiyo.
Samson Mbwambo ambaye ni miongoni mwa wakulima waliokuwa wanafanya shuguli za kilimo katika eneo husika amedai si rahisi Viongozi wa Wilaya mfano ya Monduli kugawa ardhi ya Wilaya ya Ngorongoro halafu mahakama ikaridhia jambo hilo.
Alidai kuwa hawajaridhika na hukumu hiyo kwa kuwa Jaji MASARA kwa kuwa aliegemea ushahidi wa upande mmoja kwani baadhi ya viongozi wa kijiji cha Landanai walipeleka ushahidi mbele yake na wanahisi hakuuzingatia kitendo ambacho wanahisi haki yao imepindishwa na huenda kuna harufu ya rushwa.
Post A Comment: