Mathew Gyunda mmoja wa wakulima katika Kijiji cha Nkungi wilayani Mkalama akikagua mimea ya mtama iliyopandwa kwenye shamba lake la mfano kijijini hapo,
Baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Makutupora wilayani Manyoni wakiwa katika picha ya pamoja kwenye moja ya Shamba la mfano kijijini hapo.
Na Abby Nkungu, Singida
SHIRIKA la Maendeleo la Uholanzi (SNV) limepanga kutumia jumla ya Euro milioni 39 (takriban Sh bilioni 107.3) kati ya Julai 2018 na Mei 2023 katika utekelezaji wa Mradi wa kilimo himilivu kinachotegemea hali ya hewa kwenye nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
Ofisa Ufuatiliaji wa Mradi huo Kanda ya Kati, Geoffrey Isote alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima Shambani yaliyofanyika kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Nkungi wilayani Mkalama mkoani Singida na Makutupora wilayani Manyoni.
Alisema kuwa kwa hapa Tanzania Mradi huo unatekelezwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Katavi, Mbeya na Songwe, Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida pamoja na mkoa wa Mtwara ambapo jumla ya wakulima 100,000 wanatarajiwa kufikiwa ndani ya kipindi hicho cha miaka mitano.
"Lengo letu kuu ni kuboresha mnyororo wa thamani katika mazao ya mtama, viazi mviringo, alizeti na maharage. Tunamlenga mkulima; hasa wa hali ya chini ili ahame kutoka kilimo cha mazoea na kwenda kilimo tija kwa kuongeza kipato chake kwa kutumia eneo dogo kuvuna mazao mengi na yenye ubora" alieleza Isote.
Meneja Mradi wa Musoma Food Co Ltd, Samson Msigwa, anayetekeleza Mradi wa kilimo himilivu cha zao la mtama katika wilaya za Mkalama na Manyoni mkoani Singida alisema kuwa Kampuni yake iliamua kuomba kutekeleza Mradi huo baada ya kubaini kuwa mahitaji ya zao hilo yalikuwa makubwa kuliko wakulima wanavyoweza kuzalisha.
"Miaka mitatu iliyopita kulikuwa na soko kubwa la mtama lakini uzalishaji ukawa mdogo na wa kiwango duni; hivyo tukaona umuhimu wa kumsaidia mkulima kupata mbegu bora, pembejeo sahihi, namna bora ya kupanda, kuvuna na hatimaye kununua mazao yake ili kumwepusha na adha ya kutafuta soko" alieleza Msigwa na kuongeza;
Katika kutekeleza mradi huu, tumeanzisha mashamba darasa kwenye baadhi ya vijiji ambapo wakulima wa vijiji vingine hupata fursa ya kuja kujifunza na kuiga. Hata hivyo, tunakusudia kupanua wigo wa mashamba darasa hayo kwenye vijiji vingi zaidi ili hatimaye tuweze kumfikia kila mkulima".
Ofisa Kilimo wa wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kwenye hafla hiyo kijijini Makutupora alikiri kuwa ujio wa Musoma Food Co ltd katika utekelezaji wa mradi huo umekuwa mkombozi kwa wakulima kwenye kuhamasisha na kutatua changamoto zao mbalimbali.
Aidha, aliwataka wakulima wa Makutupora na vijiji vya jirani kutumia kikamilifu fursa za ujio wa treni ya mwendo kasi (SGR) ambayo itapita eneo hilo huku Ofisa kilimo wa wilaya ya Mkalama, Seleman Msunga akisema kuwa mashamba darasa yamesaidia kupunguza pengo la mahitaji ya maafisa ugani wa kilimo kwenye wilaya hiyo.
Baadhi ya wakulima, akiwemo Mathew Gyunda, Stephen Msengi, Joyce Msengi na Hosea Kingu wa kijiji cha Nkungi wamelishukuru Shirika la SNV kwa kuleta mradi huo kijijini hapo kwa kuwakomboa kutoka kilimo duni na kuwapeleka kwenye kilimo cha kisasa chenye tija.
Kadhalika, walisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo walikuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa mbegu bora, ukosefu wa mbejeo, kutokuwepo soko la uhakika na elimu duni juu ya kilimo cha kisasa miongoni mwa wananchi.
"Kabla ya ujio wa mradi huu nilikuwa naambulia magunia 4 hadi 5 tu ya mtama kwa ekari moja lakini sasa navuna magunia 12 hadi 15 kwa eneo hilo hilo. Nawashukuru sana SNV pamoja na Musoma Food kwa kunifungua macho na kunionesha njia" alieleza Mathew Gyunda.
Post A Comment: