Na Mathias Canal, WazoHuru-Geita
Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa kiwanda cha Kusafisha Madini cha Mkoani Geita kitaongeza na kuchangamsha uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla wake.
Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko jana tarehe 8 Mei 2021 wakati akiweka Jiwe la Msingi katika kiwanda cha kusafisha madini cha GGR akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita.
Waziri Biteko amesema kuwa kiwanda hicho cha kisasa na cha kwanza cha aina yake barani Afrika kimekusudia kuimarisha nyanja za kusafisha dhababu nchini jambo litakaloimarisha soko la uhakika la uuzaji wa madini na kuiwezesha Benki kuu kununua madini yenyewe.
Amesema kuwa ni fahari kubwa katika sekta ya madini kwani uwekezaji huo ni mkubwa na muhimu utakaokijibu ndoto za serikali katika kuwakomboa wachimbaji wadogo wa madini.
Mhe Biteko amewaasa wachimbaji kuwa na ushirikiano na kupendana kwani uchumi wa nchi hauwezi kuimarika kwa baadhi ya wachimabji kuwachukia waliofanikiwa.
“Nasikitika kuna vijiwe vimegawanyika kazi yao kusuka majuku na kuwachukia wengine waliofanikiwa, Ushindeni ubaya kwa wema, aliyefanikiwa tumuombee Mungu amsogeze mbele” Amekaririwa Waziri Biteko
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Gabriel Robert amesema kuwa dhahabu inayouzwa katika mkoa huo imeamsha ari kwa wawekezaji kuanza kuwekeza katika sekta mbalimbali jambo linaloimarisha uchumi wa mkoa.
Amesema kuwa mkoa wa Geita pamoja na mambo mengine lakini ni sehemu sahihi kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya madini.
Awali akisoma taarifa ya kiwanda cha kusafisha madini cha GGR Kaimu Mkurugenzi wa Bodi Mhandisi Athuman Mfutakamba amesema kuwa kiwanda hicho kilipewa leseni ya kusafisha dhahabu No RFL 001/2019 iliyotolewa na Wizara ya Madini tarehe 16 Julai 2019 na kina uwezo wa kusafisha 400 kg kwa siku na kufikia tani 200 kwa mwaka kwa kiwango cha juu kabisa na kukidhi kufikia kiwango cha usafi wa asilimia 999.9 na 999.5
Amesema kampuni imejiimarisha ipasavyo kutekeleza wajibu huo kwa kufunga vifaa/mashine za kusafisha dhahabu vya kisasa na vyenye viwango vya hali ya juu vinavyokidhi viwango vya kimataifa.
MWISHO
Post A Comment: