Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa nne-kushoto waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tabora,  Wizara ya Nishati na  REA, baada ya kuzindua rasmi usambazaji wa umeme kwa kila kitongoji nchini uliofanyika katika Kitongoji na Kijiji cha Ufuruma,  wilayani Uyui,  Mkoa wa Tabora.



Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga (kushoto kwa Mwenyekiti), wakicheza pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Nishati na REA, kufurahia uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme katika kila Kitongoji nchini, uliofanyika katika Kitongoji na Kijiji cha Ufuruma,  wilayani Uyui,  Mkoa wa Tabora.


Transfoma ikiwa imesimikwa katika kijiji cha Ufuruma, wilayani Uyui ikiwa ni utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini unaofanywa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini nchini kote.


Na Dotto Mwaibale 

 


TANZANIA ni kinara kwa usambazaji umeme vijijini katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga wakati akizungumza katika kipindi maalumu cha Mizani kinachorushwa na Runinga ya Taifa (TBC). 

Akizungumzia dhima, alisema taasisi hiyo ya Serikali ilianzishwa kwa sheria namba 8 ya mwaka 2005 ambayo ilitoa madhumuni ya kuanzishwa wakala huo ili kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo vijijini, ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira kutokana na nishati ya kuni iliyokuwa inatumika kutokuwa rafiki kwa mazingira.  

"Lengo kuu la utunzaji mazingira hayo kwa kutumia nishati hiyo ya umeme ilikuwa ni kuyatunza vizuri ili dunia iwe mahali pazuri pa kuishi," alisema Mhandisi Maganga.  

Alisema utekelezaji rasmi wa sheria hiyo ulianza Mwaka 2008 licha ya kuwa miradi hiyo ilianza Mwaka 2007 ambapo vijiji 518 kwa Tanzania nzima vilianza kupata huduma ya umeme kati ya vijiji 12,268 na kufikia mwaka huu 2021 takribani vijiji 10,400 vimekwisha pata umeme sawa na asilimia 84. 

"Juhudi kubwa zilifanyika toka Mwaka 2008 hadi sasa zaidi ya vijiji 10,400 sawa na asilimia 84 kati ya vijiji 12,268 vilivyopo hapa nchini vimepata umeme ambapo vijiji chini ya 2,000 bado havijapata umeme," alisema Mhandisi Maganga.  

Alisema kwa sasa REA imeandaa Mradi Mwingine wa Usambazaji Umeme Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambao umechukua vijiji vyote vilivyosalia na kuwa tayari wamepata wakandarasi wa mradi huo na ambao ulizinduliwa Machi 15 mwaka huu na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wilayani Igunga mkoani Tabora na kuwa wanatarajia kati ya Julai na Disemba 2022 vijiji vilivyobakia vitakuwa na umeme.  

Mhandisi Maganga alisema siri ya mafanikio hayo makubwa ni kutokana na Serikali kuwekeza fedha Shilingi Trilioni 3.4 kwa REA na kuwa toka mwaka 2015 hadi sasa ni zaidi ya Shilingi trilioni 2.8 zimekwisha tumika.  

Alisema kutokana na usimamizi mzuri wa REA pamoja na Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO) wametekeleza miradi mikubwa ya REA Awamu ya Pili, REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza na miradi mingine ikiwemo ya kuvipatia umeme vijiji vyote vinavyopitiwa na Mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya umeme kutoka Iringa kupitia Dodoma, Singida, Tabora hadi Shinyanga wa kilovoti 400 na kuwa vijiji vyote vinavyopitiwa na njia hiyo vimepata umeme.     

 Alisema kwa wakati wote utekelezaji wa mradi huo REA wameimarisha usimamizi na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na TANESCO na ambao ndio wasimamizi wakubwa wa miradi  hiyo.  

Alisema juhudi hizo za kuhakikisha wananchi wanapata umeme zinaenda sanjari na utoaji wa elimu juu ya matumizi bora ya nishati hiyo.  

Alisema kuanzishwa kwa Viwanda vya kuzalisha vifaa vya umeme hapa nchini vimechangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kufufua fursa za ajira ambapo zaidi ya wafanyakazi 4,000 wameajiriwa.  

Akichangia mada hiyo, Mhandisi Deogratius Nagu ambaye ni Mhandisi Miradi kutoka REA, alisema miradi hiyo imewanufaisha wananchi kwa kufungua fursa za ajira kwa wakandarasi kuingia mikataba ya ajira na wananchi inakotekelezwa miradi hiyo ikiwa ni moja ya takwa la kisheria.  

Mhandisi Nagu alisema mbali na kutoa ajira hizo umeme huo umesaidia kuinua huduma za kiuchumi na kijamii kwa kupeleka umeme huo mashuleni, Zahanati, kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo  na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima vijijini ikiwa ni tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walisafirisha mahindi lakini kwa sasa wanasafirisha unga. 

Mhandisi Nagu aliipongeza Serikali kwa kuzalisha vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo hapa nchini jambo lililoharakisha utekelezwaji wa miradi hiyo tofauti na awali ambapo vifaa hivyo vilikuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi.


Share To:

Post A Comment: