Na Mwandishi wetu, Arusha
Timu ya wataalamu kutoka Tanzania imekutana na timu ya wataalamu kutoka Kenya Jijini Arusha kujadili njia za kuondoa vikwazo visivyo vya kibiasha baina ya Nchi hizo kwani vimekuwa vikiathiri biashara, mkutano wa leo Mei 26, 2021 ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Biashara wa pande zote mbili utakaofanyika tarehe 29 Mei 2021.
Mkutano wa leo utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 28 Mei 2021 na baadaye mkutano wa Mawaziri tarehe 29 Mei 2021. Mkutano huo utahitimishwa kwa mawaziri wa Kenya na Tanzania kufanya ziara katika mpaka wa Namanga tarehe 30 Mei, 2021 kujionea shughuli za biashara zinavyofanyika katika mpaka huo.
Ujumbe wa Tanzania katika timu wataalam umeongozwa na Mkurugenzi wa Mtangamano wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu wakati ujumbe wa Kenya umeongozwa na Bw. Michael Mandu, Mkuu wa Biashara baina ya Nchi na Nchi, Idara ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali.
Mkutano wa wataalamu umetoa fursa ya kujadili masuala yote yanayokwamisha biashara baina ya pande zote mbili ambapo masuala yaliyowasilishwa na Kenya kujadiliwa ni pamoja na kutotoa upendeleo kwa sigara, maziwa, bidhaa za nyama, kutoka Kenya, tozo ya kuingia kwa wafanyabiashara (business pass) kufanya kazi za muda mfupi za kitaalamu.
kwa upande wa Kenya, baadhi ya masuala ambayo Tanzania imewasilisha kujadiliwa ni kuongezwa bei ya vinywaji baridi (uplifting) kutoka Tanzania, kutoza ushuru wa forodha bidhaa za glass, kuzuia mahindi kutoka Tanzania, bei kubwa ya ushuru wa stempu katika bia, kubadili mfumo wa uingizaji mizigo mikubwa ambapo gharama za uingizaji mizigo Kenya zimeongezeka na kuathiri biashara.
Katika kutekeleza maagizo ya Wakuu wa nchi (Tanzania na Kenya) mawaziri wa seka husika kutoka watakutana na kujadili juu ya vikwazo hivyo katika mkutano wao utakaofanyika tarehe 29 Mei, 2021 jijini Arusha.
Tarehe 4 – 5 Mei, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alifanya ziara rasmi nchini Kenya ambapo katika ziara hiyo Mhe. Samia Hassan Suluhu na Mwenyeji wake Mhe. Uhuru Kenyatta pamoja na mambo mengine, walielekeza Mawaziri wa Biashara wa pande zote wakutane na kujadili vikwazo vya kibiashara ambavyo vinaathiri biashara kwa lengo la kuviondoa.
Post A Comment: